SERIKALI KUIMARISHA MINADA YA KIMATAIFA YA MIFUGO NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha na kuimarisha Minada ya Kimataifa ya Mifugo katika maeneo ya kimkakati nchini, ikiwemo Jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara, kwa lengo la kukuza biashara ya mifugo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafugaji na wafanyabiashara.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 18, 2026, Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Mwikabe Waitara, ambaye alihoji ni lini Serikali itaanzisha Minada ya Kimataifa ya Mifugo katika jimbo hilo.

“Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha minada hiyo kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya mifugo katika eneo la Tarime Vijijini pamoja na ukaribu wake na mipaka ya nchi jirani, hali inayotoa fursa kubwa za biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi.” Alisema Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha, Dkt. Bashiru aliongeza kuwa  Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo na kuwahamasisha wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali kutumia Mnada wa Mpakani wa Magena kama mnada wa kimataifa, kutokana na eneo hilo kuwa na sifa stahiki za kijiografia na kibiashara.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilitumia jumla ya shilingi milioni 175.65 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika mnada huo, ikiwemo mazizi, kipakilio, birika la maji pamoja na vyoo, ambapo ujenzi wake ulikamilika kwa asilimia 100.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO