SERIKALI KUANDAA MWONGOZO WA KURAHISISHA UWEKEZAJI SEKTA YA UVUVI NCHINI
Serikali imeanza mchakato wa kuandaa Mwongozo ambao utaainisha fursa mbalimbali ili kurahisisha Uwekezaji katika Sekta ya Uvuvi kwa lengo la kuongeza tija katika Sekta hiyo.
Akizungumza leo May 16, 2026 Jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakati wa Kikao kilichojumuisha Wataalam wa Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE), Bw. Samwel Mdachi amesema kikao kazi hicho ni cha kuandaa Mwongozo wa fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Uvuvi nchini.
"lengo kuu la kikao hiki ni kuandaa nyenzo itakayosaidia kutangaza na kuelezea kwa kina fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Uvuvi na uchumi wa Buluu nchini." amesema Ndg. Mdachi
Aidha, Ndg. Mdachi amebainisha kuwa Mwongozo huo unatarajiwa kuwa dira muhimu kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kwa kuwa utaonesha maeneo yenye fursa, aina za uwekezaji zinazopatikana nchini, pamoja na namna bora ya kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi, ambapo hatua hiyo inalenga kuongeza uwekezaji, kukuza uchumi wa buluu na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Vilevile, Ndg. Mdachi ameweka wazi kuwa kikao kazi hicho kimewezeshwa na Mradi wa Utekelezaji wa Rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (TASFAM), ambao unaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha maendeleo ya Sekta ya Uvuvi kupitia tafiti, uwekezaji na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.




Maoni
Chapisha Maoni