KAMATI YA BAJETI YAIPONGEZA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kusimamia na kutekeleza vyema ujenzi wa mradi wa kielelezo wa bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko unagharimu shilingi Bilioni 280 ambo kukamilika kwake kunakadiriwa kuzalisha ajira 30,000 katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya uvuvi nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Mashimba Ndaki kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo, wakati wa kikao cha uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko na Ununuzi wa Meli za Uvuvi wa Bahari Kuu uliofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi jijini Dodoma Mei 06, 2026.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Ndaki alimpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na timu yake ya wataalam kwa kuweza kusimamia vyema maono ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Niwapongeze Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuendelea na mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, tusiwe na bandari ya uvuvi isiyotumika, tuharakishe ununuzi wa meli ili kuiwekezesha bandari hiyo kufanya kazi na isiwe miongoni mwa miradi isiyotumika (white elephant), kwa hiyo Mheshimiwa Waziri bado mnayo kazi ya kufanya” alisema Mhe. Ndaki.
Kuhusu Ununuzi wa Meli za Uvuvi wa Bahari Kuu, Kamati hiyo imeishauri serikali kuanza kujitegemea kwa kununua meli zake yenyewe badala ya kutegemea wafadhili ambao wamekuwa wakichelewesha ununuzi wa meli hizo kutokana na masharti yao mbalimbali.
Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa aliieleza Kamati hiyo kuwa ujenzi wa Bandari hiyo ambao umefikia asilimia 97 ambapo kwa mujibu wa mkataba, Mkandarasi wa Bandari hiyo atakabidhi bandari hiyo mnamo Mei 30, 2026 hatua itakayoifungua sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.
Aidha. Mhe. Dkt. Bashiru aliishukuru kamati hiyo kwa kuwasimamia vyema na kuwapa ushauri na miongozo na mbalimbali ambayo imekuwa msaada mkubwa katika kuiwezesha wizara yake kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa bandari na ununuzi wa Meli na ugawaji wa vizimba vya kufugia samaki pamoja na boti za kisasa sa uvuvi.








Maoni
Chapisha Maoni