DKT. MADELE AWATAKA WATENDAJI SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA UADILIFU

◾ Awataka Watendaji hao kuja na Mikakati Mudhubuti ya kudhibiti Uvuvi haramu.

◾ Abainisha Mpango wa Wizara kutenga Hekta 196,324.25 kwa ajili ya Malisho.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo na Uvuvi wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo mkubwa ili kuleta mabadiliko katika Sekta hizo mbili na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, leo Mei 25, 2026 Jijini Dodoma katika Kikao kazi kilichojumuisha Wataalam mbalimbali wa Taasisi za Serikali wa Sekta hizo mbili za Mifugo na Uvuvi, Dkt. Madele amesema lengo la Kikao hicho ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji na usimamizi wa vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, na kusaidia kutoa mwelekeo na Mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo.

"Ni matumaini yangu kuwa mtatumia jukwaa hili kujadili kwa kina mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya Sekta pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo, na kikao hiki kiwe fursa ya kujenga uelewa wa pamoja katika masuala ya Sekta, kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili namna bora ya kuimarisha utekelezaji wa shughuli za Sekta kwa uadilifu na weledi." amesema Dkt. Madele 

Aidha, Dkt. Madele amewataka Watendaji hao kujadili kwa kina na kwa undani suala la Uvuvi haramu na kuja na Mikakati ya kudhibiti Uvuvi haramu ambayo haitatumia gharama kubwa sambamba kuhamasisha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi, na jinsi ya kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo inayolenga kudhibiti magonjwa ya mifugo, ili kuongeza uzalishaji na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Vilevile, Dkt. Madele amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, imeendelea kuandaa Mipango ya matumizi bora ya ardhi iliyowezesha kutenga hekta 196,324.25 za maeneo ya malisho, na hii ni moja ya njia Bora itakayosaidia  kupunguza migogoro ya ardhi kwani wafugaji wataweza kupanda Malisho kwa ajili ya Mifugo yao.

Pia, Dkt. Madele ameweka wazi jinsi Wizara inavyoendelea kuweka Mazingira wezeshi yatakayochangia kurahisisha Utendaji kazi wa Wataalam hao wa Sekta zote mbili na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyobainishwa katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka 2026/2027.

Dkt. Madele ameelezea juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Waziri wake Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, katika kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Sekta hizo nchini ili kuongeza uzalishaji, masoko na thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, hatua ambazo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa mbari bora za mifugo na viumbemaji, kuimarisha upatikanaji wa mbegu za malisho, vyakula vya mifugo na samaki, na upatikanaji wa maji, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, kukuza masoko na biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi,  na kuimarisha afya ya mifugo, viumbemaji na mifumo ya utambuzi wa Mifugo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Nchini (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi amesema Kikao hicho kinatoa fursa kwa Watendaji wa Sekta za Mifugo na Uvuvi, ya kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wizara ikiwemo uwezeshaji wa vijana kupitia mikopo yenye masharti nafuu, uzalishaji wa malisho, uandaaji na usimamizi wa Sera, Miongozo na Mikakati ya Sekta katika udhibiti wa magonjwa ya mifugo, ukusanyaji na usimamizi wa takwimu na maduhuli, utekelezaji wa Miradi ya maendeleo, pamoja masuala ya Ukuzaji viumbe maji.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, akihutubia na wadau wa Sekta za Mifugo na Uvuvi, katika Kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Uriyo Executive Hall, Mei 25, 2026 Dodoma.

Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Nchini (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi, akitoa neno la Utangulizi, katika Kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Uriyo Executive Hall, Mei 25, 2026 Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina, akizungumza na wadau wa Sekta za Mifugo na Uvuvi, katika Kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Uriyo Executive Hall, Mei 25, 2026 Dodoma.

Picha ni baadhi ya wadau wa Sekta za Mifugo na Uvuvi, wakimsikiliza Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (hayupo pichani), katika Kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Uriyo Executive Hall, Mei 25, 2026 Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele (aliyekaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta za Mifugo na Uvuvi, katika Kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Uriyo Executive Hall, Mei 25, 2026 Dodoma.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO