DKT. MADELE ASISITIZA TAASISI ZA MIFUGO KUWAPA WAFUGAJI SULUHISHO LA KISASA NA LENYE TIJA

“Tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha wafugaji wanapata majawabu ya changamoto zinazowakabili katika sekta ya mifugo. Matarajio yao makubwa ni kuona wanapata mbari bora za mifugo, mbegu bora za malisho pamoja na huduma bora za afya ya mifugo.”

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele, wakati wa kikao chake na watumishi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kilichofanyika leo Mei 20, 2026 katika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) jijini Tanga.

Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na TALIRI, Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) pamoja na Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).

Katika hotuba yake, Dkt. Madele amesema sekta ya mifugo ina nafasi kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa, hivyo ni muhimu kwa taasisi zote za wizara kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na mshikamano ili kuhakikisha wafugaji wanapata teknolojia sahihi za ufugaji kwa wakati.

Amesema upatikanaji wa teknolojia bora za mifugo, huduma za kitaalamu pamoja na tafiti zenye matokeo ya moja kwa moja kwa wafugaji ni nyenzo muhimu katika kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wafugaji na kuchangia ongezeko la Pato la Taifa.

Aidha, Dkt. Madele ameitaka LITA kuhakikisha inaendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, maarifa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya ufugaji wa kisasa na wa kibiashara unaozingatia ushindani wa soko la ndani na kimataifa.

Pia amesisitiza umuhimu wa watumishi wa taasisi hizo kufanya kazi kwa ushirikiano, uzalendo na uwajibikaji huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi baada ya kikao hicho, Walter Mangesho Mtafiti kutoka TALIRI alimshukuru Dkt. Madele kwa maelekezo na hamasa aliyotoa kwa watumishi, akisema yameongeza ari mpya ya utendaji kazi na kuwapa mwelekeo wa kuendelea kuwahudumia wafugaji kwa ufanisi zaidi.

Bw. Mangesho amesema watumishi wa taasisi hizo wataendelea kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha teknolojia, tafiti na huduma zinazotolewa zinakuwa na mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya sekta ya mifugo na ustawi wa wafugaji nchini.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO