DKT. MADELE AAGIZA UJENZI WA SOKO LA SAMAKI KIPUMBWI, PANGANI KUKAMILIKA KWA VIWANGO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele, amemtaka mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Ujenzi wa Soko la Samaki Kipumbwi kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa huku ukizingatia viwango vya ubora vinavyokidhi mahitaji ya soko la kisasa.
Dkt. Madele ametoa maelekezo hayo leo Mei 21, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa katika eneo la Kipumbwi, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2026.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya sekta ya uvuvi kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira pamoja na kuinua uchumi wa wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi na biashara ya samaki.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji, mradi huo umefikia asilimia 52 ya utekelezaji ukiwa na gharama ya jumla ya shilingi bilioni 1.34 hadi kukamilika kwake ukihusisha ujenzi wa jengo la soko la samaki, jengo la kuhifadhia baridi na chumba cha barafu, jengo la utawala, jengo la walinzi, jengo la kupokelea umeme na jenereta, pamoja na eneo la ukusanyaji taka na kazi nyingine za miundombinu ya nje.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Kipumbwi, Mhe. Akida Bahorera ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo akieleza kuwa utakuwa chachu ya kukuza uchumi wa wananchi kupitia biashara ya samaki na shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea sekta ya uvuvi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Eng. Abdul Mustapha, amesema kampuni hiyo imepokea maelekezo yaliyotolewa na Serikali na imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokusudiwa.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi WCEC Limited kama sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya uvuvi na kuongeza ushindani wa bidhaa za uvuvi katika soko la ndani na kimataifa.


Maoni
Chapisha Maoni