DKT. BASHIRU ATAKA MKAKATI WA TASNIA YA KUKU UZINDULIWE NANE NANE 2026
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameiagiza Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Watendaji wake kuhakikisha inakamilisha uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Tasnia ya Kuku nchini na kuuzindua mkakati huo wakati wa Maonesho ya Nane Nane ya Mwaka huu 2026.
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Wadau kuhusu Kilimo cha Mikataba, Uwezeshaji wa Fedha kwa Wakulima na Maendeleo ya Vyama vya Wakulima uliofanyika jijini Dodoma leo Mei 22, 2026 ambapo ameeleza kuwa kukamilishwa na kuzinduliwa kwa mkakati huo kutasaidia kuirasimisha tasnia ya kuku ambayo ina mchango mkubwa kwa uchumi na usalama.
"Tatizo Kubwa tulilonalo pamoja na sekta hii kuwa kubwa, ni sekta ambayo haijarasimishwa wala kupewa hadhi inayostahili, ndio maana ndani ya wizara tunaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya sekta ya Kuku, Napenda kuelekeza Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wataalam wenzake nahitaji mkakati huo uzinduliwe Katika sherehe za Nane nane" amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Kuhusu mkutano huo wa wadau Balozi Dkt. Bashiru alitoa rai kwa taasisi za fedha kuongeza mikopo nafuu kwa vijana na wanawake waliopo katika minyororo ya thamani ya mahindi, soya, chakula cha mifugo na kuku na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha sera, mifumo ya kifedha, huduma za ugani na miundombinu ya masoko ili kuweka mazingira bora kwa wawekezaji na wakulima.
Awali Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rigwuza amesema uzalishaji wa vyakula vya mifugo kwa mwaka 2025/2026 ulifikia Tani 897,750 kati hizo vyakula vya kuku ni tani 610, 470, nguruwe tani 197,505 na tani 89 ni kwa ajili ya ng'ombe, mbuzi na Kondoo ambapo kwa sasa mahitaji ya Soya kwa ajili ya vyakula vya mifugo ni takriban tani 275,000 ikilinganishwa na uzalishaji wa sasa ya soya nchini ambayo ni tani 13,585.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Bi. Kissa Chawe amesema kutokana na mahitaji ya zao la soya kuongezeka nchini, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeandaa mkakati wa kuendeleza zao hilo unaotarajiwa kuzinduliwa hivi Karibuni ili kuimarisha mnyororo wa thamani.






Maoni
Chapisha Maoni