DKT. BASHIRU AAGIZA KUFANYIKA TATHMINI MIUNDOMBINU YA KUFUGIA SAMAKI - NANE NANE
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kufanya tathmini ya miundombinu ya kufugia samaki kutoka kwa Mwekezaji Hawa Fish Farm ili eneo hilo litumike kwa ajili ya Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT Uvuvi).
Balozi Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo leo Mei 21, 2026 wakati alipotembelea na kukagua Mabwawa ya Kufugia Samaki ya Mwekezaji Hawa Fish Farm yaliyopo Viwanja vya Nane Nane vya John Malecela jijini Dodoma, ambapo mwekezaji huyo amesema anaondoka na kwenda kuwekeza sehemu nyingine.
"Hatuwezi kuendesha shughuli za kiserikali zinazohusu watu bila kuwa karibu nao na kurahisisha mawasiliano, Nataka maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Viumbe maji kwa nini tumechelewa kumpa majibu mwekezaji huyu kutokana na mapendekezo yake?, Pia ifanyike tathmini ya miundombinu hii kama inafaa kwa shughuli gani? amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha, Balozi Dkt. Bashiru ameongeza kwa kuitaka idara hiyo kuja na wazo mbadala la kuyatumia mabwawa hayo baada ya mwekezaji kuondoka eneo hilo, akisisitiza kuwa kwa sasa kuna Mradi wa BBT unaotekelezwa na Wizara yake, hivyo ifanyike tathmini ya jinsi miundombinu hiyo inavyoweza kutumia kwa ajili ya Programu hiyo.
Kwa mujibu wa Bi. Hawa Gondwe ambaye ni Mwekezaji na Mkurugenzi wa Hawa Fish Farm alimweleza Balozi Dkt. Bashiru kuwa aliwasilisha andiko la kupewa fidia ya miundombinu hiyo ili eneo hilo lichukuliwe na serikali kwa ajili kujenga Kituo cha Kuzalisha Vifaranga vya Samaki Kanda ya Kati ambapo hadi sasa takriban Samaki 30,000 wamepandikizwa kwenye mabwawa hayo.



Maoni
Chapisha Maoni