BWAWA LA LITA MILIONI 1.2 LAJENGWA TALIRI KUIMARISHA UZALISHAJI WA MALISHO YA MIFUGO

Katika jitihada za kuimarisha uzalishaji wa malisho ya mifugo na kuongeza uwezo wa wafugaji kukabiliana na athari za ukame, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Kaskazini imefanikiwa kujenga bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 1.2 za maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji katika eneo la shamba darasa la uzalishaji wa malisho ya mifugo.

Mradi huo unatekelezwa kupitia programu ya kuwajengea uwezo wafugaji na kuimarisha mifumo ya ufugaji kwa familia za kifugaji sambamba na kuchangia uendelevu wa usalama wa chakula nchini.

Bwawa hilo lina uwezo wa kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa shughuli za umwagiliaji katika shamba darasa lenye ukubwa wa ekari moja kwa kipindi cha hadi miezi mitatu bila kujazwa tena. Hatua inatarajiwa kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa malisho hata katika vipindi vya ukame vinavyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya mifugo kwa kutumia teknolojia na mifumo ya kisasa ya uzalishaji.

“Uwepo wa bwawa hili unatoa fursa kwa wafugaji kujifunza kwa vitendo mbinu bora za uzalishaji wa malisho pamoja na matumizi sahihi ya mifumo ya kisasa ya umwagiliaji, jambo litakalosaidia kuongeza tija katika ufugaji,” amesema Dkt. Madele.

Aidha, Dkt. Madele amesisitiza kuwa uwekezaji katika uzalishaji wa malisho ni moja ya njia muhimu za kuhakikisha mifugo inapata lishe bora na kuongeza uzalishaji kwa wafugaji.

Akizungumzia mkakati wa baadaye wa matumizi ya bwawa hilo, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Kaskazini, Dkt. Heriel Massawe amesema bwawa hilo litasaidia shughuli za umwagiliaji wa malisho katika eneo la ekari 300 lililotengwa kwa ajili ya uzalishaji wa malisho na mbegu za malisho ya mifugo.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Mradi huo, Bi. Mwanavita Jambia amesema mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Serikali ya Ujerumani (GIZ) kupitia Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kilimo ya Argentina (INTA) kwa gharama ya shilingi milioni 105.5. 

Bi. Mwanavita amesema mradi huo unalenga kusaidia shughuli za utafiti, kuongeza uwezo wa TALIRI katika uzalishaji wa mbegu na malisho ya mifugo pamoja na kuwajengea uwezo wafugaji kupitia mafunzo ya vitendo kuhusu uzalishaji bora wa malisho.

Vilevile Bi. Mwanavita ameongeza kuwa mbali na ujenzi wa bwawa hilo, mradi umefanikiwa kutekeleza shughuli nyingine mbalimbali ikiwemo kujenga uzio wa waya katika eneo la ekari mbili, kusafisha eneo la ekari 10 na kuondoa visiki pamoja na kuanzisha shamba darasa lenye ukubwa wa mita za mraba 3,200 kwa ajili ya mafunzo na majaribio ya uzalishaji wa malisho ya mifugo.

Muonekano wa bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 1.2 za maji lililojengwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa malisho ya mifugo kupitia mfumo wa umwagiliaji. Ujenzi wa bwawa hilo umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Serikali ya Ujerumani (GIZ) kupitia Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kilimo ya Argentina (INTA) kupitia mradi wa kuwajengea uwezo wafugaji na kuimarisha mifumo ya ufugaji kwa familia za kifugaji.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO