SHILINGI BIL. 9.5 ZATENGWA KUTOA MIKOPO YA BOTI ZA KISASA ZA UVUVI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Katika bajeti ya mwaka 2025/2026, imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 9.5 kwa ajili ya kutoa mikopo ya boti za kisasa za uvuvi 100, boti saidizi 76, na vifaa vyake kwa masharti nafuu kwa wavuvi na wakuzaji viumbemaji.

Hayo, yameelezwa leo Aprili 20, 2026 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani wakati wa Kipindi cha Maswali na Majibu  Bungeni Jijini Dodoma, alipokuwa ajibu swali la Mbunge wa Nyasa Mhe. John John Nchimbi lililohoji  ni lini Serikali itatoa mikopo nafuu ya Boti za Uvuvi za Fiber kwa Wavuvi wa Wilaya ya Nyasa?

“Mikopo hiyo itatolewa kwa wananchi wa mwambao wa Bahari ya Hindi, Maziwa Makuu na madogo, mabwawa na mito ambapo takribani wananchi 2,100 watanufaika moja kwa moja ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, ajira na kipato” alisema Mhe. Kamani.

Aliongeza kuwa Mikopo hiyo inalenga kutoa vifaa na pembejeo muhimu za ufugaji samaki kwa vizimba, zana za uvuvi, ufugaji wa kuku, ufugaji wa nguruwe, ufugaji wa mbuzi na kondoo, miundombinu ya ubaridi, uchakataji wa dagaa pamoja na mwani katika maeno yote ya wavuvi hapa nchini wakiwemo wavuvi wa Wilaya ya nyasa. 

Hatua ya utoaji wa mikopo kwa vijana  ni utekelezaji wa ahadi  ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa Shilingi Bilioni 200 kwa vijana ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani  kwa ajili ya kufanya biashara ndogo, za kati na kampuni changa.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO