PROF. SHEIKH AAGIZA UFUATILIAJI WA UBORA WA VIFARANGA VYA SAMAKI

Na Chiku Makwai, WMUV

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh, ameielekeza Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kuimarisha ufuatiliaji wa ubora na idadi ya vifaranga vya samaki vinavyozalishwa na kusambazwa kwa wanufaika kwenye shamba la Katabe, mkoani Kigoma.

Ametoa maelekezo hayo leo Aprili 15, 2026, wakati wa ziara yake ya kutembelea na kusikiliza changamoto za wanufaika wa mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika eneo hilo.

Prof. Sheikh amesema Serikali ina mpango wa kufanya utafiti wa kitaalamu ili kupata vifaranga bora vya samaki nchini kote kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hatua itakayochangia samaki kukua kwa haraka na kuzaliana kwa wingi zaidi kulingana na mabadiliko ya mazingira.

“Ubora wa vifaranga ni msingi muhimu wa kuongeza uzalishaji  katika ufugaji wa samaki kwa  njia ya vizimba, kukuza kipato cha wafugaji, pamoja na kuhakikisha mafanikio ya miradi ya maendeleo katika sekta ya uvuvi” amesema Prof. Sheikh 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikundi cha wanufaika wa mradi huo, Bw. Suleiman Ibrahim, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni kushuka kwa uzalishaji wa samaki ikilinganishwa na awali, hali inayochangiwa na kupungua kwa ubora wa vifaranga pamoja na ucheleweshaji wa upatikanaji wa chakula cha samaki.

Naye Afisa Uvuvi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw. Subugu Masami, amesema tayari wameanza kuchukua hatua za kuboresha ubora wa vifaranga na kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu mbinu bora za usimamizi na ufuatiliaji wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO