BI. MEENA AHIMIZA USHIRIKIANO KUINUA SEKTA YA MIFUGO
Na, Fausta Njelekela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena amekutana na Watendaji wakuu wa Taasisi na Wataalam wa Sekta ya Mifugo kwa lengo la kujadili kwa pamoja jinsi ya kuongeza ushirikiano baina ya viongozi na Wataalamu wa Sekta hiyo ili kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili wataalam hao katika utendaji kazi ili kuleta tija katika Sekta hiyo.
Akizungumza wakati wa Kikao hicho cha majadiliano na Wataalamu wa Sekta hiyo, yaliofanyika leo Aprili 15, 2026 Katika Ukumbi wa Ofisi ya Wizara Jijini Dodoma, Bi. Meena amesema Ushirikiano Katika Sekta ya Mifugo utaleta mbinu bora za kutatua changamoto zinazoikumba Sekta ya mifugo Kwa kutumia wataalamu walioko kwenye maeneo ya wafugaji.
"Ushirikiano baina ya viongozi na Wataalamu wa Sekta ya Mifugo utasaidia kutambua changamoto zilizopo na kuzitatua, Ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo." amesema Bi. Meena
Aidha, Bi. Meena, ameweka msisitizo kwa Watendaji hao kujikita katika kuongeza ushirikiano ili kutafuta mbinu bora za kuvumbua changamoto na njia bora za kutatua changamoto hizo zinazoikumba Sekta ya mifugo kwakutumia wataalam walioko kwenye maeneo ya wafugaji.
Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabiani Madele, amesema Ushirikiano Katika Sekta ya Mifugo ni muhimu ikiwa viongozi na wadau wa kitaaluma wataungana pamoja ili kuendeleza Sekta hii ili kuimarisha na kuikuza.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini, Dkt. Benezeth Lutege, amesema kuwa Wizara inatakiwa kuwa na jukumu la kusimamia dawa, chanjo na vifaa tiba na kufuatilia changamoto zinazoikumba Sekta ya Mifugo ili kuweza kuzitatua kwa haraka zaidi.
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA), Prof. Erson Karimuribo, amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikumba Sekta ya Mifugo ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana, changamoto ya kuhudhuria mafunzo ya wanagenzi, na ameishukuru Wizara kwa kuwakutanisha wataalam hao wa Sekta ya Mifugo pamoja ili kubainisha na kuchakata changamoto za mifugo ili kuweza kuzitatua.






Maoni
Chapisha Maoni