TASFAM YATOA MAFUNZO KUONGEZA THAMANI ZAO LA MWANI MKOANI LINDI

Na. Martha Mbena.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kupitia Mradi Kuendeleza na Kusimamia Uvuvi wa Baharini na Ukuzaji viumbe maji kwa njia endelevu nchini Tanzania (TASFAM) Umeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha Mwani,  Ufugaji Jongoo Bahari, uanzishwaji wa Vikundi pamoja na Kanuni za Ukuzaji viumbe maji kwa wanufaika wa mradi huo ndani ya Manispaa ya Lindi, Mkoani Lindi.

Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo yaliyofanyika Machi 26,2026 Mkoani humo Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Happy Kapinga amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakulima wa zao la mwani pamoja wafugaji wa jongoo Bahari.

"Leo tumekuja hapa  Mkoani Lindi, Kata ya Mchinga kwa ajili ya kutekeleza malengo ya mradi wa TASFAM  ambapo  takribani wakulima 600 tunatarajia wapate uelewa katika Ukuzaji Viumbe maji kwa mkoa wa Lindi", Amesema Bi. Kapinga.

Aidha, Kapinga  ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano, hivyo utasaidia katika ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na  Taifa kwa Ujumla.

Kwa upande wake Mkulima wa zao la mwani Bi. Mwajuma Mohamed kutoka kata Ya Mchinga, ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia mradi wa TASFAM kwa kuwapatia mafunzo ya mbinu bora za kuongeza thamani kwa zao hilo, jambo litakalochochea uchumi kutokana na zao hilo 

"Tunaishukuru Wizara kupitia mradi huu wa TASFAM wametupa mafunzo  ili tuweze kuongeza thamani katika kilimo chetu cha Mwani  tunaomba mafunzo haya yawe endelevu", Amesema Bi. Mwajuma.

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mradi wa TASFAM inaendelea kutoa mafunzo kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa vikundi vya wakulima wa zao la mwani na wafugaji wa Jongoo Bahari.

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Happy Kapinga akionyesha bidhaa zitokanazo na mwani wakati wa mafunzo kwa Wakulima wa Mwani na wafugaji wa  Jongoo Bahari yaliyotolewa kupitia mradi wa TASFAM Machi 26, 2026 Mkoani Lindi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Dkt. Stanford Mwakatage (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na timu ya wataalamu wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wataalamu wa Mkoa wa Lindi mara baada ya timu hiyo kutembelea ofisini kwa lengo la kujitambulisha na kueleza lengo la kutoa mafunzo kwa Wakulima wa Mwani na Wafugaji Jongoo Bahari kupitia Mradi wa TASFAM kwa mkoa wa Lindi, Machi 26,2026.

Wakulima wa Mwani wakifatilia kwa makini, wakati wa  mafunzo ya kuwajengea uelewa Wakulima wa Mwani na Jongoo Bahari, yanayotolewa  kupitia Mradi wa kuendeleza na kusimamia Uvuvi wa Baharini na Ukuzaji viumbe maji kwa njia endelevu nchini Tanzania (TASFAM), katika Kata ya Mchinga, Machi 26, 2026 Lindi.


Afisa Uvuvi, wa kituo cha ukuzaji viumbe maji  Ruhila-Ruvuma, Mr Justine Ndayeze akitoa mafunzo kuhusu kanuni za ukuzaji viumbe maji kwa wanufaika wa mafunzo yanayotolewa na mradi wa TASFAM kwa wakulima wa zao la mwani pamoja wafugaji wa jongoo Bahari wa mkoa wa Lindi, Machi 26,2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO