KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA NCHINI

Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula limekutana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kujadiliana namna ya kuongeza uzalishaji katika sekta hizo ili kuimarisha  usalama wa chakula nchini.

Mwenyekiti wa Baraza hilo na Waziri Mkuu Mstaafu  Mhe. Mizengo Pinda  ameongoza kikao hicho leo Machi 24, 2026 katika Ukumbi wa Kilimo Four Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa  baraza hilo limekuwa likiimarisha ushirikiano wa wadau na sekta binafsi katika kuongeza uzalishaji na kuzihimiza Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kufanya kazi kwa umoja ili kuyafikia malengo ya kuongeza uzalishaji ifikapo Mwaka 2030.

“Malengo haya yanatupeleka 2030 leo hii 2026 unaona kabisa muda sio rafiki kwa hiyo nguvu kubwa sana inahitajika lakini tukiwa wamoja hatutashindwa kuyafikia” amesema Mhe. Pinda.

Akisoma taarifa ya Mpango wa Kuongeza Uzalishaji wa Chakula Nchini Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt. Florence Turuka amesema dhamira ya serikali katika sekta ya mifugo ni kuongeza uzalishaji wa nyama ya ng’ombe kutoka tani 742,000 za Mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani 1,000,000 ifikapo 2030 na uzalishaji wa maziwa kufikia lita bilioni 5 ifikapo 2030 kutoka lita bilioni 3.4 za Mwaka 2021/2022.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema Wizara yake imeendelea kusimamia sekta za mifugo na uvuvi katika kuimarisha usalama wa chakula na kumuomba mwenyekiti wa baraza hilo kuisaidia Wizara ya Mifugo na Uvuvi  kuwa wasimamizi wa mfumo mzima wa afya ya mifugo ikiwemo udhibiti wa dawa za mifugo nchini.

“Kwa bahati mbaya sasa hivi shughuli za udhibiti wa dawa za mifugo uko chini ya TMDA, kidogo hili linakaukakasi na TMDA iko chini ya Wizara ya Afya, lakini dunia imebadilika sasa hivi  mchakato ni zaidi ya kudhibiti dawa lakini TMDA inakuwa haifanyi usimamizi wa kisayansi wa afya ya mifugo” amesema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo amesema kuna umuhimu wa serikali kuifanya kwa ushirikiano Programu ya Vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuleta ufanisi ambao utawanufaisha vijana  kiuchumi.


Mwenyekiti wa Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula Mhe. Mizengo Pinda akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo na Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kilichofanyika Leo Ukumbi wa Kilimo Four Machi 24, 2026 Jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumia sekta za mifugo na Uvuvi wakati wa kikao cha Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula na Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kilichofanyika Leo Ukumbi wa Kilimo Four Machi 24, 2026 Jijini Dodoma.

Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo akielezea hatua zinazochukuliwa na Wizara yake kuimalisha usalama wa chakula wakati wa kikao  cha Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula Kilichofanya Ukumbi wa Kilimo Four Machi 24, 2026 Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula na baadhi ya Watendaji wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi  wakiwa kwenye Kikao hicho kilichofanyika Ukumbi wa Kilimo Four Machi 24, 2026 Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula Mhe. Mizengo Pinda (Kulia) akiteta Jambo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally wakati wa kikao kilichofanyika Kilimo Four Jijini Dodoma leo Machi 24, 2026

Wajumbe wa Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Kilimo na Chakula, Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye Picha ya Pamoja baada ya Kikao leo Machi 24, 2026 Eneo la Kilimo Four, Jijini Dodoma


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO