DKT. BASHIRU AZINDUA MWONGOZO WA KITAIFA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Nchini (BMUs) ili kulinda rasilimali hizo ambazo ni muhimu katika kukuza uchumi na kuimarisha usalama wa chakula.

Mhe. Dkt. Bashiru amezindua mwongozo huo leo Machi 25, 2026 wakati akifunga Mkutano wa Siku Mbili wa Ngazi ya Juu Kuhusu Mustakabali wa Uendelevu na Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi na Uchumi wa Buluu aliofanyika Jijini Dodoma, na kutoa rai kwa Wataalam, Viongozi na Wadau wa Sekta ya Uvuvi nchini kutafuta mbinu shirikishi katika kukabiliana na uvuvi usiofuata sheria.

“Nimefanya ziara Kanda ya Ziwa nimeona kuna watu wanafanya ubunifu wa uhalifu kwa kubadilisha nyavu halali kufanya uvuvi usiofuata sheria, utaratibu wa namna ile  huwezi kudhibiti kwa Polisi, utakuwa na Polisi wangapi ?, njia pekee ya kufanikiwa ni kuwa na mbinu shirikishi na kuelimishana bila kuchoka, kwa hiyo huu mwongozo usiishie kwenye makaratasi” alisema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Hifadhi ya Mazingira Duniani (TNC) Bi. Lucy Magembe amesema shirika hilo  na wizara ya mifugo na uvuvi hufanya ushirikishwaji wa wavuvi katika uhifadhi na kusimamia rasilimali za uvuvi, kupitia BMUs katika kuimarisha uvuvi endelevu na uchumi wa buluu nchini.

“Tumekuwa tukitoa sayansi na elimu ya uvuvi bora, kushirikiana na wananchi kupunguza uvuvi haramu ili kudumisha uvuvi endelevu” alisema Bi. Magembe.

Awali Naibu Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya uvuvi Prof. Mohamed Sheikh  amesema ulinzi wa rasilimali uvuvi ni jukumu la kila mtu na kwamba vikundi takriban 700  vya BMUs nchini vimekuwa vikishirikiana na wananchi  katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa( Wapili Kulia) akizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi wakati wa Mkutano na Wadau wa Sekta ya Uvuvi leo Machi 25, 2026 Jijini Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa( Wanne Kulia), Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, TNC  na wawakilishi wa BMUs wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya Uzinduzi wa  Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi leo Machi 25, 2026 Jijini Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Kulia) akiwashuhudia Katibu Mkuu Bi. Agnes Meena (Kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Hifadhi za Mazingira Duniani (TNC) Bi. Lucy Magembe (Kushoto) wakitia saini kwa ajili ya ushirikiano wa Wizara na Shirika hilo katika uhifadhi wa rasilimali za uvuvi, hafla iliyofanyika Leo Machi 25, 2026 Jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akifunga Mkutano wa Ngazi ya Juu Kuhusu Mustakabali wa Uendelevu na Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi na Uchumi wa Buluu uliofanyika Gerwill Hotel Jijini Dodoma Machi 25, 2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena akitoa neno la Utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufunga Mkutano wa Ngazi ya Juu Kuhusu Mustakabali wa Uendelevu na Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi uliofanyika leo Machi 25, 2026 Jijini Dodoma

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Hifadhi za Mazingira Duniani (TNC) Bi. Lucy Magembe akieleza jinsi shirika hilo linavyoshirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhifadhi, kulinda na kuendeleza Rasilimali za Uvuvi wakati wa Mkutano na Wadau wa sekta ya Uvuvi leo Machi 25, 2026 Jijini Dodoma


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO