DKT. BASHIRU AKUTANA NA MAAFISA WAFAWIDHI KUJADILIANA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekutana na Maafisa Wafawidhi wa Vituo vya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kwa lengo la kujadili kwa pamoja  jinsi kusimamia rasilimali hizo na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wataalam katika utendaji kazi wao.

Katika Majadiliano  hayo na Maafisa Wafawidhi yaliofanyika leo Machi 25, 2026 Jijini Dodoma Mhe. Balozi Dkt. Bashiru aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena, Naibu Katibu Mkuu(Uvuvi) Prof. Mohamed Sheikh, Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi Nchini, Dkt. Baraka Sekadende na Wataalam wengine wa Wizara.

Pamoja mambo mengine yaliyojadiliwa kwenye Kikao hicho, msisitizo mkuu ulijikita katika kutafuta mbinu bora za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi hususan kudhibiti utoroshwaji wa samaki na dagaa katika maeneo ya mipakani, uimarishaji wa uvuvi endelevu pamoja na kukabiliana na uvuvi usiofuata sheria, lakini kuangalia mianya inavyosababisha upotevu wa mapato yatokanayo na  mazao ya uvuvi.

Aidha, Balozi Dkt. Bashiru amewatoa hofu na kuwatia moyo maafisa hao huku akiwaahidi kuyabeba masuala yote ya kisera na kuyapeleka katika ngazi za maamuzi  yenye tija ili kurahisisha ufanyaji kazi za usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa hapa nchini.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena alisema kuwa maafisa wafawidhi wamekuwa chachu ya kufikia lengo la  makusanyo ya maduhuli yatokanayo na sekta ya uvuvi ambapo  2024/2025 wizara ilitakiwa kukusanya Shilingi Bil. 33 lakini  maafisa hao walichangia kukusanya shilingi Bil. 32 sawa na asilimia 99 ya lengo.

Bi. Meena amesema katika Mwaka wa Fedha 2025/ 2026 Wizara imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 43  ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi bilioni 26 imekusanywa kwa mchango mkubwa wa maafisa wafawidhi ikiwa sawa na asilimia 59 ya lengo ambalo wizara iliyopangiwa na serikali kuu.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO