WAUZAJI VYAKULA VYA MIFUGO WATAKIWA KUSAJILI NA KUHUISHA VYETI VYAO VYA USAJILI

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Februari 27, 2026, imefanya ukaguzi wa maeneo ya kuuza, kuzalisha na kuhifadhi rasilimali za vyakula vya mifugo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma, kwa lengo la kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa vinakuwa na ubora na wadau wanafata taratibu, miongozo, kanuni na sheria.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bi Theodata Sallema, amesema pamoja na kukagua ubora wa vyakula vinavyozalishwa, Pia Wizara inaangalia kama wafanyabiashara wanafanya biashara kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kusajili maeneo yao ya biashara.

"Ukaguzi  huo, unalenga kubaini namna vyakula vinavyozalishwa,  kuhifadhiwa na kusambazwa ili kuhakikisha havileti madhara kwa mifugo wala kwa mlaji wa mazao yatokanayo na mifugo hiyo".Bi. Sallema

Aidha, amebainisha kuwa Wizara inaendelea kuwasaidia wadau kujiunga kwenye mfumo wa utoaji vibali wa kielektroni yaani MIMIs, ili kurahisisha mchakato wa maombi ya vibali na kuongeza utoaji wa huduma.

Bi. Sallema amewataka wafanya biashara ya vyakula vya mifugo kusajili maeneo yao ya biashara na kuhuisha leseni zao kwa wakati ili kuepuka kuvunja sheria, akisisitiza kuwa lengo la ukaguzi huo si kuadhibu bali ni kutoa elimu kwa wadau ili wafate taratibu zilizopo kwani kwa kufanya hivyo watalinda afya za  mifugo na kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kukua kwa kuzingatia viwango na ubora.

Idara hiyo itaendelea na ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha vyakula vya mifugo na rasilimali za vyakula vya mifugo zinaboreshwa ili kuwanufaisha wafugaji pamoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi  wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bi. Theodata Sallema (wa kwanza kulia), akitoa  maelekezo kwa msimamizi wa kiwanda cha kuzalisha chakula cha mifugo wakati wa ukaguzi wa ubora na uhalali wa leseni, leo tarehe 27 Februari 2026.


Baadhi ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (kulia), wakizungumza na mmiliki wa duka la pembejeo za mifugo wakati wa ukaguzi wa vibali, leseni na ubora wa vyakula vya mifugo katika moja ya maduka Mkoani Dodoma , leo tarehe 27 Februari 2026.

Msimamizi wa kiwanda cha kuzalisha chakula cha mifugo (kulia) akitoa maelezo kwa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati wa ukaguzi wa vibali, leseni  na ubora wa vyakula vya mifugo, leo tarehe 27 Februari 2026 Mkoani Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bi. Theodata Sallema (katikati),  akitoa  elimu juu ya usafi na utunzaji wa vyakula vya vya mifugo wakati wa ukaguzi wa ubora na uhalali wa leseni, leo tarehe 27 Februari 2026 Mkoani Dodoma.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO