VCT YAWATAKA WATOA HUDUMA ZA AFYA YA WANYAMA KUJISAJILI
Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) limewataka wamiliki wa Vituo vya kutoa Huduma za Wanyama pamoja na Wataalam wake kujisajili katika Baraza ili waweze kutambulika na Baraza hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), wakati wa Ukaguzi wa Vituo mbalimbali vya kutolea Huduma za Afya ya Wanyama pamoja na Wataalam wake, leo Februari 24, 2026 Mkoani Dar es Salaam, Mkaguzi wa Baraza hilo, Dkt. George Mtinda, amesema takwa la kusajili Wataalam na Vituo vya Huduma za Afya ya Wanyama ni takwa la kisheria ambalo linamtaka Mtaalam au mtoa Huduma hizo kujisajili ili kutambulika na Baraza.
"hii ni moja ya utekelezaji wa Sheria ya Veterinari SURA 319, ambayo inawataka Wataalam na Vituo vya kutolea Huduma hizo kujisajili ili kujua kama wamekidhi vigezo katika kutoa huduma.” amesema Dkt. Mtinda
Aidha, Dkt. Mtinda amebainisha kuwa ni vyema kuhakikisha watoa Huduma wote wa Afya za Wanyama wanasajili Vituo vyao pamoja na kutumia Wataalam wenye sifa na waliojasiliwa na Baraza ili kuepuka athari za sitofahamu kwa Mifugo na Wanyama.
Vilevile, Dkt. Mtinda amesema operesheni Maalum inaendelea nchini kwa ajili ya zoezi la ukaguzi wa shughuli za utoaji wa Huduma za Afya ya Wanyama katika Vituo mbalimbali ili kuangalia kama Huduma hizo zinatolewa kuendana na Sheria ya Veterinari Namba 16 ya 2003.
Pia, Dkt. Mtinda amesema kwa Wataalam au wamiliki wa Vituo vya Huduma za Afya ya Wanyama wanaoshindwa kufuata Sheria za Baraza na kutojisajili watachukuliwa hatua mara moja ikiwemo kufungiwa kutoa Huduma hizo.
Dkt. Mtinda amewataka wafugaji kutumia Vituo vilivyosajiliwa na Wataalam waliokidhi vigezo na kuthibitishwa na Baraza hilo ili kuepukana na athari kwa Mifugo yao na kuenea kwa magonjwa ya Mifugo.




Maoni
Chapisha Maoni