SERIKALI YAANZISHA MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA UVUVI
Na. Stanley Brayton
◾Vizimba vya Bahari kuanza.
◾Wizara kuanzisha Mikakati ya Kimageuzi Sekta ya Uvuvi yatajwa.
◾ Vifaranga vya Samaki maji baridi na maji chumvi kupandikizwa.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa kufuga samaki kwa njia ya Vizimba katika bahari, mpango ambao utasaidia kuongeza Uzalishaji wa Samaki chumvi na Masoko nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh, katika ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga alipotembelea Kituo cha Ukuzaji Viumbemaji Machui kwa ajili ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa kuzalisha chakula cha Samaki aina ya Viroboto maji (Atemia), leo Februari 27, 2026, amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa sasa ipo katika utekelezaji wa kukuza Viumbemaji kwa njia ya Vizimba kupitia bahari, mpango ambao utaongeza tija katika Sekta ya Uvuvi.
"Mpango huu ni mpango mzuri ambao utekelezaji wake unategemea kuanza kufanyika ndani ya miezi mitatu katika maeneo mbalimbali yenye bahari nchi.” amesema Prof. Sheikh
Aidha, Prof. Sheikh amesema Wizara ipo kwenye hatua ya kuanzisha programu ya Kitaifa ya ufugaji Samaki kwa ajili ya kuzalisha Vifaranga Bora vya Samaki na Viumbe vingine vya maji ya baridi ikiwemo kaa na jongoo bahari ili kuongeza Uzalishaji katika Sekta.
Vilevile, ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Idara ya Ukuzaji Viumbemaji (DAQ) kushirikiana katika kupandikiza vifaranga vya kaa na jongoo bahari na kuzalisha kwa wingi Vifaranga vya Samaki maji baridi na maji chumvi ili wananchi waweze kufuga na wavuvi waweze kupata mbegu hizo kwa wingi na urahisi zaidi.
Pia, Prof. Sheikh ameiagiza Taasisi ya TAFIRI na Idara ya Uzalishaji Viumbemaji (DAQ) kuandaa Mkakati wa Mageuzi wa Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji kwa mwaka 2026/2050 (National Fish Breeding Programs na Fisheries Fisheries and Aquaculture Transformation Strategy 2026-2050), ambao utaleta mabadiliko katika Sekta ya Uvuvi na unaoendana na Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Prof. Sheikh amewataka wananchi kutumia fursa hii adhim ili kuweza kunufaika na Ufugaji Samaki wa Vizimba kupitia bahari.






Maoni
Chapisha Maoni