MRADI WA MALISHO J-CRISD WAANZA KUTEKELEZWA CHAMWINO

Mradi wa Uoteshaji wa Malisho ya Mifugo aina ya Juncao na Ustahimilivu wa Tabianchi (J-CRISD) unaofadhiliwa na IDN Norway umeanza kutekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na IDN Africa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, ambapo wafugaji wanapatiwa mafunzo ya kulima malisho kwa njia ya mashamba darasa.

Uzinduzi wa utekelezaji wa mradi huo umefanyika Februari 19, 2026 katika shamba la mfugaji Mayunga Mashishanga lililopo Kata ya Mpayungwa, Katika uzinduzi huo, Afisa Usimamizi wa Nyanda za Malisho Bw. Boniphace Shija, alimwakilisha Mkurugenzi wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo na kutoa wito kwa wafugaji kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo.

“Zao hili tunalolipanda linalenga kusaidia upatikanaji wa malisho ya kutosha, pamoja na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, nitumie fursa hii kulishukuru Shirika la IDN Africa kwa kuwezesha utekelezaji wa shughuli hii, hivyo wafugaji mtoe ushirikiano,” alisema Bw. Shija.

Aidha, Meneja wa Shamba la Malisho la Serikali Vikuge lililopo Pwani, Bw. Ruben Ngailo, amesema mbegu aina ya juncao hukua haraka endapo itatunzwa vizuri, na inaweza kuchukua miezi minne hadi sita kuwa tayari kupandikizwa katika maeneo mengine au kuchakatwa kuwa saileji.

Baada ya kupatiwa mafunzo ya uoteshaji na mbegu za Juncao, Bw. Mayunga Mashishanga amesema ukame umekuwa ukiathiri wafugaji kwa kusababisha upungufu wa malisho, hivyo mpango wa kuhamasisha ulimaji wa malisho utasaidia kuongeza upatikanaji wa chakula cha mifugo na kuboresha uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa IDN Africa Kanda ya Afrika Mashariki, Jonathan Kifunda amewahimiza maafisa ugani kuhakikisha usambazaji sahihi wa mbegu kwa wafugaji katika kata za Itiso, Mvumi, Makang’wa na Chilonwa, ambapo wafugaji 20 watapatiwa mbegu kwa ajili ya mashamba darasa yatakayosaidia kuwafundisha wengine, huku mradi ukitarajiwa kuwanufaisha wafugaji 500 katika kipindi chote cha utekelezaji.

Afisa Usimamizi wa Nyada za Malisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Boniphace Shija ( wa tatu kushoto) akivuta Kitambaa kuashiria uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa Uoteshaji Malisho ya Mifugo na Ustahimilivu wa Tabianchi (J - CRISD), uliofanyika Februari 19, 2026  Kata Mpwayungu, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Afisa Usimamizi wa Nyada za Malisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Boniphace Shija ( wa pili kushoto) akiongoza zoezi la upandaji wa mbegu za malisho aina ya juncao kwenye shamba la mfugaji (Mayunga Mashishanga) wakati wa uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa J - CRISD, uliofanyika Februari 19, 2026  Mpwayungu, Chamwino, Dodoma.

Meneja wa Shamba la Malisho Vikuge Bw. Ruben Ngailo (wapili kulia) akiwaeleza wafugaji njisi ya kupanda Malisho

Picha ya Pamoja Wataalam na Wafugaji wa Kata ya  Mpwayungu baada ya uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa Uoteshaji Malisho ya Mifugo na Ustahimilivu wa Tabianchi (J - CRISD), uliofanyika Februari 19, 2026 kwenye shamba la mfugaji ( Mayunga Mashishanga) Chamwino, mkoani Dodoma.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO