DKT. BASHIRU AGEUKA ‘MBOGO’ NARCO KUKOSA DAWA ZA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kushirikiana na Idara ya Huduma ya Mifugo na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa ajili ya kuangalia upatikanaji wa dawa za mifugo kuhudumia ranchi hiyo  iliyopo Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma na wafugaji wengine kwa ujumla kuzunguka eneo hilo.

Agizo hilo amelitoa leo Februari 26, 2026 wakati akizungumza na kusikiliza changamoto za wafugaji na wawekezaji wadogo waliopewa vitalu ndani ya NARCO Kongwa ambapo Dkt. Bashiru amemwagiza pia Katibu Mkuu wa Wizara yake, kusimamia umoja kwa watendaji pamoja na taasisi zake ili kuiendeleza sekta ya mifugo na uvuvi.

“Wizara hii ni moja na Waziri wake ni mmoja na aliyemteua Waziri wenu ni Rais huyo mmoja halafu tunashindwa kufanya kazi kama timu moja kwanini?. Watu wa chanjo wako kwenye ofisi yangu, chanjo zinatoka ofisini kwangu, Mkuu wa Madakatari wote wa mifugo yuko kwangu, anayedhibiti dawa za mifugo nchi nzima yuko ofisini kwangu, lakini Ranchi za Taifa, Kampuni yake ambayo nayo ipo ofisini kwangu nayo haina dawa hizo, naelekeza kwa mara ya mwisho jambo hilo, Katibu Mkuu awakumbushe  watendaji ndani ya wizara jukumu lao la kufanya kazi kama timu moja” alisema Balozi Dkt. Bashiru.

Hatua hiyo imejiri baada ya Dkt. Bashiru kupokea changamoto kutoka kwa  wafugaji wakiwakilishwa na Bw. Kedmond Maskini ambaye ni mfugaji mpangaji wa vitalu vya NARCO Kongwa kukosa huduma ya Dawa za mifugo eneo hilo jambo linalowafanya kushindwa kuhudumia mifugo yao.

Aidha, Waziri Balozi Dkt. Bashiru alisema kumekuwepo na utapeli katika suala la upatikanaji wa dawa za mifugo hivyo amelekeza huduma hiyo ipatikane katika taasisi ya wizara ikiwemo NARCO kwa upande Kongwa ili kuwaondolea adha wanauopata wafugaji kutafuta dawa za mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally (Kulia) akisalimiana na Wafugaji na Wawekezaji wadogo katika vitalu vilivyoko NARCO Kongwa baada ya kufanya majadiliano nao ya kuendeleza sekta ya mifugo leo 26 Februari 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Katikati) akizungumza na  Wafugaji na Wawekezaji wadogo wa Vitalu vya NARCO Kongwa leo Februari 26, 2026.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Simon Mayeka akiwashukuru Wafugaji na wawekezaji wadogo wa vitalu vya NARCO baada ya mkutano na Waziri wa Mifugo na Uvuvi leo Februari 26, 2026.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Mohamed Zuberi Mbwana akitoa shukran kwa Waziri Balozi Dkt. Bashiru Ally baada ya majadiliano na wafugaji waliopangishwa vitalu NARCO Kongwa yaliyofanyika leo tarehe 26 Febrauri 2026.

Wafugaji na Wawekezaji Wadogo wa Vitalu Vilivyoko NARCO Kongwa wakiwa kwenye mkutanao baina yao na Waziri wa Mifugo na Uvuvi leo 26 Februari 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO