Nav bar

Jumatano, 28 Januari 2026

DTK. BASHIRU AITAKA TADB KUONGEZA WIGO WA MIKOPO SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa( Mb.) amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TABD) na kufanya mazungumzo  na yanayolenga kuendeleza ushirikiano kati ya wizara na benki hiyo  na kuitaka kuendeleza miradi ya sekta za mifugo na uvuvi.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo 27 Januari 2026 katika ofisi ndogo ya wizara hiyo iliyopo Kambarage Tower Jijini Dodoma, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TADB alifika kujitambulisha kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Benki ya TADB katika kuendeleza sekta za Mifugo na Uvuvi.

Katika Mazungumzo hayo Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameipongeza Benki ya TADB kwa jinsi inavyoshirikiana na wizara na kuiagiza  kupanua wigo wa kuwasaidia wafugaji wadogo kupata mikopo nafuu ili waweze  kuendeleza miradi yao, pamoja na kuongeza ushiriki wa Taasisi za kifedha kupitia TADB katika kutoa mikopo kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Frank Nyabundege  amempongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kwa kuteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  na kuahidi kuongeza kasi ya utoaji mikopo kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi hasa kwenye miradi inayowalenga vijana na wanawake.

Aidha,  Bw. Nyabundege aliwasilisha taarifa  fupi kuhusu ushiriki wa TADB katika Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi  nchini ambapo kupitia TADB kama  Benki ya  Kisera  inashirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuleta maendeleo katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi ikiwemo  Benki kutoa mikopo ya mradi wa boti, ufugaji samaki kwa njia ya vizimba na  mikopo ya vijana kupitia Programu ya BBT mifugo. 

Kupitia mikopo ya miradi ya boti na vizimba TADB ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 34.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi Bilioni 29.83 kimetolewa kwa wanufaika 5,932 katika mikoa 16 hapa nchini. 

Aidha, TADB kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kutoa jumla ya  boti 219 na vizimba 536 kwa wanufaika wa miradi.  Aidha, kwa kupitia mradi wa vijana wa BBT Mifugo, kiasi cha Shilingi Milioni 847.3 kimetolewa kwa wanufaika 106 kwa miradi ya mikopo isiyo na riba. 

Bw. Nyabundege aliongezea kuwa TADB  imewasilisha ushiriki wake katika kutoa mikopo katika Sekta ndogo ya Maziwa nchini kupitia Mradi wake wa TI3P ambapo kiasi cha Shilingi  bilioni 40 kimetolewa kwa wafugaji na  wasindikaji wa maziwa nchini. Aidha, kupitia mradi wa TI3P TADB imefanikiwa kurekebisha na kujenga vituo 23 vya kukusanya maziwa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.1 kwa kushirikiana wafugaji,Wizara, Halmashauri na wasindikaji wa maziwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wa kwanza, kushoto) akitoa maelekezo  kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Frank Nyabundege (wa pili, kulia) alipofika kujitambulisha kwa waziri leo Januari 27, 2026 Ofisi ndogo ya Wizara iliyopo Kambarage Tower, Jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa  akitoa maelekezo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) leo Januari 27, 2026 Ofisi ndogo ya Wizara iliyopo Kambarage Tower, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Frank Nyabundege akitoa taarifa kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya sekta za mifugo na uvuvi alipofika kujitambulisha kwa waziri leo Januari 27, 2026 Ofisi ndogo ya Wizara iliyopo Kambarage Tower, Jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni