Nav bar

Jumanne, 22 Oktoba 2024

PROF. SHEMDOE AONGOZA TIMU YA WATALAAM KUTOKA TANZANIA MKUTANO WA IOTC BANGKOK, THAILAND

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe aongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa 13 wa Kamati ya Wataalam ya Vigezo vya Mgawanyo wa Mavuno ya Samaki aina ya Jodari na Jamii zake (13th Technical Committee on Allocation Criteria - TCAC13) ya Kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi (Indian Ocean Tuna Commission (IOTC) unaofanyika Bangkok, Thailand kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba 2024. 

Prof. Shemdoe ameongoza Timu hiyo ya wataalam akiwa ameongozana na Maafisa wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) akiwemo Dkt. Emmanuel Sweke, Mkurugenzi Mkuu wa DSFA.

Katika kuhakikisha mgawanyo huo wa samaki unakuwa sawa kwa nchi wanachama, kamati hiyo ya IOTC iliundwa  katika kikao chake cha 14 kilichofanyika Busan, Korea tarehe 1 hadi 5 Machi, 2010 kwa lengo la "kujadili vigezo vya ugawaji kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali za Jodari katika Bahari ya Hindi na kupendekeza mfumo mzuri wa mgao.

 Aidha,  kwa takribani miaka 13 sasa Kamati hiyo imeendelea kujadili mfumo utakaowezesha usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za samaki aina ya Jodari na jamii zake kwenye Bahari ya Hindi.

Kwa kuzingatia mikakati ya Tanzania katika kukuza Uvuvi wa bahari kuu,Tanzania imepiga hatua kubwa  ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko na ufufuaji wa mashirika ya uvuvi (TAFICO na ZAFICO) na matarajio ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi kwa Ujumla wake.

Prof.Shemdoe amesema kuwa "Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu tumeendelea kutetea msimamo wetu  kama Nchi ya Mwambao inayoendelea (Developing Coastal State) wa haki yake ya msingi ya kupata kiasi cha samaki kinachostahili pindi ambapo mfumo wa ugawaji wa rasilimali za Jodari utakapopitishwa na kuanza kutumika." Alisema Prof.Shemdoe.

Vilevile, haki hii ya msingi imeainishwa katika Sura ya 16 ya Mkataba wa kuanzishwa kwa IOTC (IOTC Agreement) ya mwaka 1993, Mkataba wa Uhifadhi na Usimamizi wa Samaki wanaohama hama (Highly Migratory Fish Stocks and Highly Straddling Fish stocks), “United Nations Fish Stock Agreement - UNFSA) wa mwaka 2001 na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (United Nations Convention on the Law of the Sea - UNCLOS) ya mwaka 1982.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa DSFA Dkt. Emmanuel Sweke (Kushoto) Katika Mkutano wa IOTC nchini Bangkok,Thailand Jana tarehe 21 Oktoba 2024.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akifuatilia wasilisho  katika Mkutano wa IOTC unaoendelea nchini Bangkok Thailand Jana tarehe 21 Oktoba, 2024. Lengo la Mkutano huo ni kuhusu namna bora ya Kufanya mgawanyo wa Kiasi cha Samaki aina ya Jodari katika Bahari ya Hindi kwa nchi wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania.



Jumatatu, 21 Oktoba 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI MKUTANO WA JUKWAA LA TASNIA YA KUKU NA NDEGE WAFUGWAO KWA NCHI ZA SADC

Na. Stanley Brayton

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 17 Octoba, 2024 Serena Hotel jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza leo tarehe 11 Oktoba, 2024  jijini Dodoma, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdala Ulega, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe, amesema lengo la mkutano huo ni kukuza fursa za ajira nje na ndani ya nchi pamoja na kujadili na kubadilishana uzoefu wa sekta hiyo  na nchi za SADC.

“mkutano huo utatoa nafasi kwa Tanzania kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo katika Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa hizo katika nchi za SADC na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za SADC katika Tasnia hiyo” amesema Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameshukuru uongozi wa awamu ya sita uliochini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele na kufungua fursa za wawekezaji katika sekta za uzalishaji ikiwemo Tasnia ya Kuku.

Vilevile, Prof. Shemdoe amesema tukio hilo litaambatana na maonesho ya kitaifa ya Tasnia ya kuku na ndege wafugwao yatakayofanyika 18-19 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar Es Salaam.

Prof. Shemdoe amesema, mgeni Rasmi katika mkutano huo ni Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko.

Aidha, Prof. Shemdoe amewakaribisha wadau wote wa ufugaji kuku na watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika matukio haya, kwani jukwaa hili na maonyesho haya ni bure na hayana gharama.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, kuhusu uwepo wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) ambao utafanyika tarehe 16 - 17 Oktoba, 2024 katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar es Salaam na kufuatiwa na maonesho ya Kitaifa ya Tasnia ya kuku na ndege wafugwao yatakayofanyika Oktoba 18 -19, 2024 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ni katika Ukumbi wa Wizara - NBC, Oktoba 11, 2024, Dodoma





TANZANIA NA IRAN ZA SAINI HATI SABA ZA MAKUBALIANO ILI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Na. Stanley Brayton

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran zimesaini hati saba  za makubaliano ili kukuza diplomasia ya uchumi baina ya mataifa hayo mawili.

Hafla ya kusaini hati hizo za makubaliano imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, tarehe 19 Oktoba, 2024, katika mkutano wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Kilimo wa   Jamhuri ya Kiislaam ya  Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh walishuhudia zoezi hilo la uwekaji saini hati hizo lililohusisha Wizara za Kisekta, baadhi ya Taasisi za Umma na Taasisi binafsi. 

Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliohusisha Viongozi wa ngazi za juu za Serikali za nchi hizo, wakiwemo Mawaziri, Mhe. Balozi Kombo amemshukuru Mhe. Golamreza Nouri kwa jitihada zake za kuimarisha ushirikiano wa uwili na azma yake katika kuongeza maeneo ya ushirikiano yakiwemo Mifugo na Uvuvi,  biashara na  uwekezaji,   kilimo, nishati, ulinzi   na   usalama na elimu. Maeneo mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Iran yatahusisha sekta ya afya, sayansi na teknolojia, na utamaduni. 

Hati hizo za makubaliano zilihusisha hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   na Wizara ya Kilimo ya   Jamhuri ya Kiislam ya   Iran, kuhusu ushirikiano katika sekta ya Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Mifugo na Uvuvi  ya Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Iran kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya ya wanyama; na hati ya makubaliano baina ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Michezo na Vijana ya Iran. 

Hati nyingine za Makubaliano zilisainiwa baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira, na Watu wenye ulemavu ya Tanzania na Wizara ya Ushirika, Kazi na Maendeleo ya Jamii ya Iran kuhusu ushirikiano katika kazi, ajira na usalama wa raia.Taasisi   za Serikali zilizotia saini   hati za makubaliano ni pamoja   na Kikosi cha Uokozi  na Zimamoto, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, na Kitengo kinachoshughulikia masuala ya moto cha Iran, kuhusu ushirikiano katika huduma za zima moto na uokozi. 

Aidha katika hafla hiyo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilitia saini hati  ya makubaliano na Taasisi ya Uendelezaji  Biashara ya Iran kuhusu ushirikiano  katika kukuza na kutangaza biashara kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Kwa upande wa sekta   binafsi, Taasisi ya Biashara, Viwanda  na   Kilimo ya Tanzania ilisaini hati ya  makubaliano na Taasisi  ya Biashara,  Viwanda  na  Kiimo ya Iran kuhusu   ushirikiano katika uanzishwaji wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya nchi hizo mbili. 

Akitoa neno la shukrani   wakati wa kuhitimisha   kikao hicho, Naibu   Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki   anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb) amewashukuru Mawaziri, Viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi pamoja na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mkutano huo wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran, kwani umeziwezesha pande zote mbili kufikia malengo ili  kukuza  diplomasia na ushirikiano  wa kimataifa.

Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran, ulianza rasmi tarehe 16 Oktoba 2024, na ulitanguliwa na kongamano la biashara, kikao cha ngazi ya  Wataalam   na   Maafisa   Waandamizi   kutoka   Tanzania   na   Iran   kilichoandaa   agenda   za kuiamarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo pamoja na Kikao cha ngazi ya juu ya Viongozi wa nchi hizo wakiwemo Mawaziri, ambacho kiliidhinisha  na kutia saini Hati za Makubaliano ya pamoja kwa manufaa ya nchi hizo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (kulia aliyesimama), na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislaam ya  Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh (kushoto aliyesimama) wakionesha hati za makubaliano ya ushirikiano baada ya kuzisaini, ni katika Mkutano wa tano wa Tume ya pamoja ya kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran, ambayo umefanyika katika Ukumbi wa JNICC, Oktoba 19, 2024. Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (kulia aliyekaa na kusaini), akisaini hati za makubaliano ya ushirikiano na Iran, ambazo hati hizo zimehusisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, ni katika Hafla ya utiaji saini hati za makubaliano ya ushirikiano wakati wa Mkutano wa tano wa Tume ya pamoja ya kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran, ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa JNICC, Oktoba 19, 2024. Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislaam ya  Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh


Jumatano, 16 Oktoba 2024

NWM-DKT. BITEKO: ASILIMIA 55 YA KAYA NCHINI ZINAFANYA SHUGHULI ZA UFUGAJI KUKU

Na. Stanley Brayton

Naibu Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko amesema asilimia 55 ya kaya nchini zinafanya shughuli za ufugaji kuku uliopelekea ongezeko la uchumi jumuishi unaolenga kujenga kesho iliyo bora.

Amyasema hayo leo tarehe 16 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Serena Hotel Dar Es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya Kuku na Ndege wafugwao kwa Nchi za Kusini mwa Afrika.

“Tasnia hii imeajiri zaidi wanawake na vijana, vilevile inazalisha malighafi za viwanda, inachangia usalama wa chakula na lishe na upatikanaji wa fedha za kigeni” 

Aidha Dkt. Bitteko amesema lengo la mkutano huo ni kujadili na kubadilishana uzoefu kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na kubainisha fursa za kimkakati zinazohusu tasnia ya kuku na ndege wafugwao.

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Ulega amesema kuwa kuku ni mifugo rafiki na mifugo hiyo haihitaji eneo kubwa katika kuitunza, inazaliana kwa haraka na haihitaji mtaji mkubwa hivyo mikakati ya uwekezaji katika Tasnia hiyo ili kuongeza ajira hususani kwa Vijana na Wanawake na kuhangia pato la taifa,

Aidha ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi kipindi wanapofanya tafiti zinazohusu mifugo na uvuvi na mazao yake ili kuepusha kuleta taharuki kwa watumiaji wa bidhaa hizo.


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, akihutubia washiriki (hawapo pichani) wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao ambalo limefanyika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, akihutubia washiriki (hawapo pichani) wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao ambalo limefanyika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza na washiriki (hawapo pichani) wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao ambalo limefanyika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (aliekaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Mashirika ya Binafsi, ni katika Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao, lililofanyika katika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam. Wa pili kulia kwa waliokaa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (aliekaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na vijana wa mnyororo wa thamani katika Tasnia ya kuku kutoka nchi Tanzania (62), Msumbiji (10) na Shirikisho la Vyama vya Kilimo Kusini mwa Afrika SACAU (10) ambao wamepongezwa leo kwa mchango wao katika Tasnia hiyo, ni katika Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao, lililofanyika katika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam. Wa pili kulia kwa waliokaa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega


Jumatano, 9 Oktoba 2024

DKT. MPANGO AZIPONGEZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KWA UTEKELEZAJI MZURI WA SHUGHULI ZAKE

Na. Stanley Brayton

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amezipongeza Sekta za Mifugo na Uvuvi kwa utekelezaji mzuri wa shughuli zake ambazo zimelenga kukuza shughuli za ufugaji na uvuvi kwa kuendana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuhudumia wananchi na kuwapa maisha Bora.

Akizungumza, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango leo Oktoba 8, 2024 katika Ziara yake wilayani Igunga, Mkoani Tabora, Dkt. Mpango amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya vizuri katika kuhakikisha mifugo bora inapatikana kwa wananchi kwa kutoa pembejeo bora kwa wafugaji na wavuvi, vilevile kutoa mikopo kwa wafugaji na wavuvi pamoja na kuwapatia mbegu bora za vifaranga vya samaki pamoja na madume Bora ya ng'ombe.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo imefanya mambo mengi sana kwa watanzania na ata katika Wilaya ya Igunga ikiwa ni kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi.

“tuna fursa ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, na ya utengenezaji wa mabwawa ya kufugia samaki pamoja na kutoa madume Bora ya ng'ombe kama mbegu”, amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, Mhe. Mnyeti amesema, Madume Bora ya ng'ombe yalishagawiwa katika baadhi ya wilaya, ikiwemo Wilaya ya Bahi, Serengeti na Bunda.

Vilevile, Mhe. Mnyeti amesema mpango huo ni endelevu hapa nchini, na Wizara inampango wa kusambaza madume hayo Bora ya ng'ombe katika wilaya zote nchini Tanzania ila yaweze kupanda ng'ombe wa kienyeji na kupata ng'ombe wengine walio Bora.


Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, akimuuliza swali Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (hayupo pichani), ni lini Wizara italeta Madume Bora ya ng'ombe Wilayani Igunga, ni katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Igunga - Tabora


Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, akijibu swali la Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpangoni (hayupo pichani), kuwa Wizara italeta Madume Bora ya ng'ombe 20 Wilayani Igunga baada ya wiki tatu, ni katika Ziara ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Igunga - Tabora


Picha ni wananchi wakimsikiliza Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora ya Oktoba 8, 2024, Igunga - Tabora


Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukene kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe Bora kwa watoto na mama wajawazito ili waweze pata Protini ya kutosha itakayowasaidia kukuza ufikiri wa mtoto na kusisitiza Maafisa kutoa elimu kuhusu lishe Bora ili jamii zielewe nini maana ya lishe bora na umuhimu wake, ni katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora


Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, akisalimia wanakijiji wa Bukene na kutoa Salamu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ni katika Ziara ya kikazi Mkoani Tabora ya Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora



 Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango (aliyeshika bomba la maji), akifungua maji kama Ishara ya Uzinduzi  na Upanuzi wa Mradi wa Maji kutoka ziwa Viktoria kwenda Bukene, ni katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora, Wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti


Picha ni Washiriki mbalimbali wakiwemo wakazi wa Bukene na Maafisa mbalimbali na Viongozi wa Serikali wakiwa katika Ziara ya kikazi Mkoani Tabora ya Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora





Jumanne, 1 Oktoba 2024

DKT. MHINA AIPA HEKO MRADI WA AgResults KWA UTEKELEZAJI MZURI

Na. Stanley Brayton

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Charles Mhina amepongeza utekelezaji wa Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa (AgResults Tanzania Dairy Productivity Challenge) kwa utekelezaji mzuri wa kukuza Sekta ya Mifugo, ususani katika kuboresha mahusiano mazuri kati ya wafugaji na maafisa wa malisho pamoja na maafisa Mifugo, na kutoa pembejeo kwa wafugaji na utoaji wa huduma za Ugani ili kukuza Sekta hii ya Mifugo. 

Akizungumza, katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa,  kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Mhina amesema anawapongeza maafisa wa Mradi wa AgResults kwani wametumia namna mbalimbali ili kuweza kuwafikia wafugaji wadogo na kuweza kuwapatia huduma mbalimbali za ugani, ikiwa ni pamoja na kutoa pembejeo za Mifugo.

“mradi huu umefika mpaka kwa wafugaji mbaimbali maeneo ya vijijini kiasi kwamba umetoa huduma kwa wafugaji na mifugo yako kwa kuboresha malisho pamoja utoaji chanjo”, amesema Dkt. Mhina

Aidha, Dkt. Mhina amesema ni wajibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha huduma zinawafikia wafugaji hadi vijijini, ikiwa ni pamoja na utoaji chanjo za mifugo na tiba kwa mifugo pamoja na pembejeo ili kuweza kuwapa huduma mbalimbali zitakazosaidia kuboresha mifugo na maisha ya wafugaji.

Vilevile, Dkt. Mhina amesema Wizara iangalie ni namna gani inaweza kuwafikia wafugaji Tanzania nzima ili kuhamasisha na kutoa mbegu Bora za madume ya ng'ombe kwa wafugaji na kuhakikisha matibabu ya mifugo yanapatikana kwa wakati.

Dkt. Mhina ametoa rai kwa maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi katika kuboresha huduma za mifugo, na kuhakikisha maziwa salama yanapatikana kwani asilimia kubwa ya watanzania hawanywi maziwa salama, na hii inatokana na maziwa mengi kuuzwa kienyeji, na mashirikiano hayo yatasaidia katika kuboresha usindikaji na utunzaji maziwa kwa njia ya usalama zaidi kiasi cha kutanua masoko nchini hadi nchi za nje.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Charles Mhina na ndiye Mgeni Rasmi, akitoa Hotuba fupi, katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa, uliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, Dodoma


Msimamizi wa Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa (AgResults Tanzania Dairy Productivity Challenge Project), Bi. Neema Mrema, akitoa Ripoti ya Utekelezaji wa Mradi wa AgResults, ni katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa, uliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, Dodoma


Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Stephen Michael, akitoa neno la Ukaribisho kwa washiriki, ni katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa, uliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, Dodoma