Nav bar

Jumanne, 22 Oktoba 2024

PROF. SHEMDOE AONGOZA TIMU YA WATALAAM KUTOKA TANZANIA MKUTANO WA IOTC BANGKOK, THAILAND

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe aongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa 13 wa Kamati ya Wataalam ya Vigezo vya Mgawanyo wa Mavuno ya Samaki aina ya Jodari na Jamii zake (13th Technical Committee on Allocation Criteria - TCAC13) ya Kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi (Indian Ocean Tuna Commission (IOTC) unaofanyika Bangkok, Thailand kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba 2024. 

Prof. Shemdoe ameongoza Timu hiyo ya wataalam akiwa ameongozana na Maafisa wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) akiwemo Dkt. Emmanuel Sweke, Mkurugenzi Mkuu wa DSFA.

Katika kuhakikisha mgawanyo huo wa samaki unakuwa sawa kwa nchi wanachama, kamati hiyo ya IOTC iliundwa  katika kikao chake cha 14 kilichofanyika Busan, Korea tarehe 1 hadi 5 Machi, 2010 kwa lengo la "kujadili vigezo vya ugawaji kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali za Jodari katika Bahari ya Hindi na kupendekeza mfumo mzuri wa mgao.

 Aidha,  kwa takribani miaka 13 sasa Kamati hiyo imeendelea kujadili mfumo utakaowezesha usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za samaki aina ya Jodari na jamii zake kwenye Bahari ya Hindi.

Kwa kuzingatia mikakati ya Tanzania katika kukuza Uvuvi wa bahari kuu,Tanzania imepiga hatua kubwa  ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko na ufufuaji wa mashirika ya uvuvi (TAFICO na ZAFICO) na matarajio ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi kwa Ujumla wake.

Prof.Shemdoe amesema kuwa "Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu tumeendelea kutetea msimamo wetu  kama Nchi ya Mwambao inayoendelea (Developing Coastal State) wa haki yake ya msingi ya kupata kiasi cha samaki kinachostahili pindi ambapo mfumo wa ugawaji wa rasilimali za Jodari utakapopitishwa na kuanza kutumika." Alisema Prof.Shemdoe.

Vilevile, haki hii ya msingi imeainishwa katika Sura ya 16 ya Mkataba wa kuanzishwa kwa IOTC (IOTC Agreement) ya mwaka 1993, Mkataba wa Uhifadhi na Usimamizi wa Samaki wanaohama hama (Highly Migratory Fish Stocks and Highly Straddling Fish stocks), “United Nations Fish Stock Agreement - UNFSA) wa mwaka 2001 na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (United Nations Convention on the Law of the Sea - UNCLOS) ya mwaka 1982.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa DSFA Dkt. Emmanuel Sweke (Kushoto) Katika Mkutano wa IOTC nchini Bangkok,Thailand Jana tarehe 21 Oktoba 2024.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akifuatilia wasilisho  katika Mkutano wa IOTC unaoendelea nchini Bangkok Thailand Jana tarehe 21 Oktoba, 2024. Lengo la Mkutano huo ni kuhusu namna bora ya Kufanya mgawanyo wa Kiasi cha Samaki aina ya Jodari katika Bahari ya Hindi kwa nchi wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni