Na. Stanley Brayton
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran zimesaini hati saba za makubaliano ili kukuza diplomasia ya uchumi baina ya mataifa hayo mawili.
Hafla ya kusaini hati hizo za makubaliano imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, tarehe 19 Oktoba, 2024, katika mkutano wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislaam ya Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh walishuhudia zoezi hilo la uwekaji saini hati hizo lililohusisha Wizara za Kisekta, baadhi ya Taasisi za Umma na Taasisi binafsi.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliohusisha Viongozi wa ngazi za juu za Serikali za nchi hizo, wakiwemo Mawaziri, Mhe. Balozi Kombo amemshukuru Mhe. Golamreza Nouri kwa jitihada zake za kuimarisha ushirikiano wa uwili na azma yake katika kuongeza maeneo ya ushirikiano yakiwemo Mifugo na Uvuvi, biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, ulinzi na usalama na elimu. Maeneo mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Iran yatahusisha sekta ya afya, sayansi na teknolojia, na utamaduni.
Hati hizo za makubaliano zilihusisha hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran, kuhusu ushirikiano katika sekta ya Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Iran kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya ya wanyama; na hati ya makubaliano baina ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Michezo na Vijana ya Iran.
Hati nyingine za Makubaliano zilisainiwa baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira, na Watu wenye ulemavu ya Tanzania na Wizara ya Ushirika, Kazi na Maendeleo ya Jamii ya Iran kuhusu ushirikiano katika kazi, ajira na usalama wa raia.Taasisi za Serikali zilizotia saini hati za makubaliano ni pamoja na Kikosi cha Uokozi na Zimamoto, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, na Kitengo kinachoshughulikia masuala ya moto cha Iran, kuhusu ushirikiano katika huduma za zima moto na uokozi.
Aidha katika hafla hiyo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilitia saini hati ya makubaliano na Taasisi ya Uendelezaji Biashara ya Iran kuhusu ushirikiano katika kukuza na kutangaza biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wa sekta binafsi, Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania ilisaini hati ya makubaliano na Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kiimo ya Iran kuhusu ushirikiano katika uanzishwaji wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya nchi hizo mbili.
Akitoa neno la shukrani wakati wa kuhitimisha kikao hicho, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb) amewashukuru Mawaziri, Viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi pamoja na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mkutano huo wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran, kwani umeziwezesha pande zote mbili kufikia malengo ili kukuza diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.
Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran, ulianza rasmi tarehe 16 Oktoba 2024, na ulitanguliwa na kongamano la biashara, kikao cha ngazi ya Wataalam na Maafisa Waandamizi kutoka Tanzania na Iran kilichoandaa agenda za kuiamarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo pamoja na Kikao cha ngazi ya juu ya Viongozi wa nchi hizo wakiwemo Mawaziri, ambacho kiliidhinisha na kutia saini Hati za Makubaliano ya pamoja kwa manufaa ya nchi hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni