Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. David Silinde amesema serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kuhakikisha wafugaji wanafuga kisasa na kibiashara ili kuongeza tija kwa wafugaji na mchango wa Sekta ya Mifugo kwenye pato la taifa.
Silinde
ameyasema hayo leo (17.06.2023) wakati akifungua mafunzo yenye Kauli Mbiu ya “Youth Bussiness Engangement Through Livestock” kwa vijana
wajasiriamali wanaonenepesha mifugo kupitia vituo atamizi, Kampasi ya LITA
Kikulula, Karagwe.
Katika kufanikisha utekelezaji
wa mpango huo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
iliandaa mwongozo ambao umeainisha majukumu ya wadau mbalimbali walioko katika
mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo. Kwa upande wa taasisi za fedha ikiwemo
mabenki, Wizara, pamoja na mambo mengine, inawategemea kusaidia kubadilisha
fikra na mitazamo ya vijana kuwa ya kibiashara ili kuweza kutengeneza fursa
nyingi zaidi za ajira kupitia sekta ya mifugo; pamoja na kuwafundisha namna ya
kuandaa mipango biashara kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza biashara zao mara
baada ya kumaliza muda wao katika Vituo Atamizi.
“Nawapongeza LITA na
Benki ya NMB kwa kutumia fursa hii kutoa mafunzo na kuwaandaa vijana wetu
kikamilifu kuwa wawekezaji na wafanyabiashara watarajiwa. Kupitia mafunzo haya
pia mnaendelea kuwandaa wateja wenu watarajiwa kupitia mikopo yenye riba na
masharti nafuu. Naamni ninyi pamoja na wadau wengine mtaendelea kutoa mafunzo
kama haya katika vituo vingine ambavyo viko chini ya Wizara yetu,” alisema
Silinde
Silinde amewataka vijana
kutokata tamaa kwa kuwa maisha ni mapambano hata pale watakapokutana na
changamoto ya aina yoyote wanatakiwa kutafuta njia ya kukabiliana nayo na sio
kukata tamaa. Vilevile amewataka vijana waliopata fursa ya kupatiwa mafunzo
kuwa mfano katika kuleta taswira na dira mpya katika taifa kupitia Sekta ya
Mifugo na Uvuvi.
Aidha, amewataka vijana
wanufaika wa mpango huo kuwa wavumilivu, wasikivu na wadadisi zaidi ili kuweza
kuzijua fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi za fedha pamoja na asasi
nyingine za maendeleo. Vijana wametakiwa kujituma zaidi ili kuweza kufikia
ndoto na maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, ya kuendelea kuongeza kipato na fursa za ajira kwa vijana na
wanawake wengi wa hapa nchini.
Mtendaji wa Wakala ya
Vyuo vya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi
kupitia LITA na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) imeanza kutekeleza
program ya Jenga Kesho iliyobora kwa vijana wetu kupitia miradi ya ufugaji
mifugo kibiashara kupitia vituo atamizi nane (8) nchi nzima. Vituo hivi viko
katika mkoa wa Tanga, Mwanza na Kagera. Tayari kuna washiriki 240 wamedahiliwa
ambapo kila mshiriki atapata fursa ya kunenepesha ng’ombe wasiopungua 40 katika
mizunguko minne ndani ya mwaka mmoja. Mzunguko wa kwanza wa unenepeshaji
umeanza ambapo ng’ombe wapatao 2,400 wamenunuliwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe,
Mhe. Julius Laizer ameishauri Wizara kuangalia uwezekano wa kutenga asilimia 20
ya maeneo ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kwa ajili ya kutumika na vijana
kwa shughuli za ufugaji ili wanapomaliza mafunzo wasihangaike kutafuta ardhi
kwa ajili ya kufugia.
Mshiriki wa Mafunzo Atamizi
katika Kampasi ya LITA Kikulula, Resti Mgonja wakati akisoma risala amesema
toka mafunzo hayo yameanza wamefanikiwa kupata elimu ya unenepeshaji kuanzia
kwenye ushiriki wa ununuzi wa ng’ombe mnadani ambapo wamenunua ng’ombe 600,
wamefanya uogeshaji wa ng’ombe ili kuwakinga na magonjwa, wamefanikiwa kuongeza
uzito wa kilo 50 kwa ng’ombe ndani ya siku 90 na kufanikiwa kufyeka maeneo kwa
ajili ya malisho takribani ekari 50.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni