Nav bar

Alhamisi, 27 Aprili 2023

SHIRIKIANENI NA MAMLAKA HUSIKA ILI MCHANGO WA SEKTA YA UVUVI UONEKANE – MHE. SILINDE

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amezisihi nchi wanachama wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuungana na mamlaka zinazoshughulikia viwanda na biashara na takwimu kuhakikisha mchango wa sekta ya uvuvi unaonekana wazi kwenye pato la Taifa la kila nchi.


Mhe. Silinde (Mb.) ametoa wito huo jijini Kampala, Uganda alipozungumza katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika  Aprili 20,2023 jijini humo.


Mhe. Silinde amesema kuwa suala hilo linatokana na ukweli kwamba mazao yanayotokana na uvuvi yanahesabiwa katika sekta za kilimo na uzalishaji na kuacha mazao mengine yakiingizwa katika mnyororo wa thamani wa sekta nyingine na kusababisha mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa nchi uonekane mdogo.


Akizungumzia ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa hilo Mhe. Silinde amesema uvuvi haramu na uvuvi uliopitiliza unahatarisha uwepo endelevu wa rasilimali za uvuvi na mazalia yake katika Ziwa Victoria.


Aidha Mhe. Silinde ameongeza kuwa taarifa zinasema kuwa idadi ya Samaki aina ya Sangara kwa mfano imepungua kwa asilimia 33 katika muda wa mwaka 2021 na 2022 nakuongeza kuwa nchi wanachama wanachama wa LVFO haziwezi kukaa pembeni na kuacha vitendo hivyo vikiendelea kushamiri kwakuwa vinaathiri mamilioni ya watu ambao maisha yao yanategemea ziwa hilo.


Amesema Ziwa Victoria linatoa maji kwa matumizi ya majumbani na kusuapoti shughuli mbalimbali za kiuchumi ukiwemo uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji katika nchi zetu na hivyo suala la ulinzi wake ni lazima kutiliwa mkazo.


“Ni wazi kuwa sekta ndogo mbili hizi ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi katika nchi zetu zote na mtakubaliana nami kuwa Uvuvi katika Ziwa hilo unatoa ajira, chakula, mapato kwa familia na kuziwezesha familia hizo kuishi pamoja na kuzipatia nchi fedha za kigeni na mapato kwa nchi na hivyo ni lazima kuziangalia kwa umakini,” alisema Mhe. Silinde. 


Mhe Naibu Waziri Silinde alitumia Mkutano huo kuipongeza Sekretarieti ya LVFO na nchi wanachama kwa kuunga mkono utekelezaji wa progrmu na miradi ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji.

Amesema wakati akizipongeza Nchi wanachama na Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) kwa kutekeleza maelekezo na maagizo yaliyotolewa na Mikutano ya Baraza la Mawaziri iliyopita amezitaka kuhakikisha hatua na jitihada za pamoja za kuwalinda Samaki aina ya sangara na rasilimali nyingine zinazopatikana katika ziwa Victoria zinaendelezwa na kuimarishwa.


“Ni wazi kuwa kumekuwa na hatua kubwa katika utekelezaji wa maagizo na maelekzo yanayotolewa na Baraza la Mawaziri, hili linonekana wazi kutokana na idadi ya miradi iliyotekelezwa huu ni ushahidi tosha kuwa sekretarieti ya LVFO iko makini katika kutekeleza maagizo yanayotolewa na Baraza la Mawaziri la sekta, nawapongeza sana,” alisema Mhe. Silinde


Mhe. Silinde pia alipongeza Kamati ya Uratibu inayoongozwa na Makatibu Wakuu kwa kuandaa vyema nyaraka za mkutano wao na hivyo kurahisisha kazi ya Mawaziri katika kikao hicho.


Katika Mkutano huo Tanzania ilikabidhi kijiti cha uenyekiti kwa Uganda na kuipongeza kwa kuchukua nafasi hiyo na hivyo kuitakia utekelezaji mwema wa majukumu yake ya kulinda rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akizungumza   wakati wa Mkutano wa TANO wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la nchi wanachama wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Kampala Aprili 20 Aprili,2023

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (wa pili kushoto ) akiwa na Mawaziri kutoka nchi za Uganda, Kenya na Burundi baada ya kumalizika kwa Mkutano wa TANO wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la nchi wanachama wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Kampala Aprili 20, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (wa pili kutoka kulia) akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa TANO wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la nchi wanachama wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Kampala  Aprili 20,2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni