Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo na kuwasilisha taarifa ya muundo na majukumu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Bwawa la kuvuna maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo la Matekwe lililopo Nachingwea, Mkoani Lindi, na taarifa ya ujenzi wa bandari ya uvuvi iliyopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi.
Baada ya kupokea taarifa hiyo mapema leo Machi 12, 2023, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. David Kihenzile alimuhakikishia Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kuwa watashirikiana bega kwa bega na Wizara ili kuiwezesha kufikia malengo yake ya kuwahudumia wananchi ili wapate maendeleo katika shughuli zao za kila siku za ufugaji na uvuvi.
Aidha, kamati hiyo inatarajiwa kufanya ziara Mkoani Lindi hivi karibuni kwa ajili ya kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifafanua jambo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma Machi 12, 2023. Kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. David Kihenzile (Mb), akitoa majumuisho baada ya kupokea taarifa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizowasilishwa kwa Kamati hiyo Machi 12, 2023.
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Sera na Mipango, Bw. Mbaraka Stambuli akiwasilisha taarifa ya Wizara kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma Machi 12, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (watano kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha kuwasilisha taarifa kwa kamati hiyo kilichofanyika jijini Dodoma Machi 12, 2023. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. David Kihenzile (Mb). Wengine ni Wajumbe wa Kamati hiyo na wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni