Nav bar

Jumamosi, 4 Machi 2023

SEKTA YA MIFUGO SMT NA SMZ ZAIMARISHA USHIRIKIANO

Na Saja Kigumbe


Serikali ya Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zaimarisha ushirikiano Ili kutatua changamoto kwenye Sekta ya Mifugo  ili kufikia uzalishaji wenye tija wa mifugo.


Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati akifungua kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ) kilichofanyika jijini Dodoma Machi 3, 2023.


‘’Tumekuwa tukishirikiana pia kwenye maeneo ya masoko kuona ni namna gani tunaweza tukaimarisha masoko ya bidhaa za mifugo kwa pande zote mbili.  Kwa hiyo ushirikiano huu unalenga kuondoa vikwazo ambavyo vinaweza kuifanya biashara ya mifugo isikue kwa haraka ,’’ alisema Dkt. Mhina


Dkt. Mhina alisema sehemu zote za Bara na Zanzibar kuna viwanda vya kuzalisha bidhaa za mifugo ikiwemo nyama, ngozi, maziwa na bidhaa nyingine hivyo ushirikiano huo utasaidia kuimarisha sekta hiyo ya mifugo.


Aliongeza kwa kusema kuwa ushirikiano huo umelenga kutatua changamoto kwenye maeneo mbalimbali hususan changamoto  za kikodi kwa kushauri mamlaka husika ziweze kufanya marekebisho ili kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi zaidi kati  ya pande zote mbili  za muungano.


"Lakini ushirikiano huu pia utatuwezesha kutumia fursa za pamoja kama zitakuwepo ikiwemo fursa za kusafirisha bidhaa za nyama kwenda nje ya nchi ili tuweze kuyafikia masoko hayo kwa kiasi kikubwa,’’ alifafanua  Dkt. Mhina.


Aidha, alibainisha kuwa  ushirikiano huo utajikita pia katika maeneo ya utafiti na mafunzo ili waweze  kujifunza kila upande ni namna gani sekta zinafanya ili kuzalisha kwa tija mifugo na bidhaa zake.


‘’Pia tutajifunza ni kwa  namna gani  wafanyabiashara na wafugaji  wa sekta binafsi wanawezeshwa kutumia fursa zilizopo kuzalisha kwa tija na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa,’’ alibainisha


Kwa upande wake,  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dkt. Omary Ali Amir  alisema wanatumia ushirikiano huo kujifunza tafiti mbalimbali na pia kujenga uwezo wa wataalam wao kupitia Tanzania bara kwa maana Tanzania bara wako mbele kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uzalishaji, Masoko, na Utafiti.


‘’Sekta ya mifugo sio ya muungano, lakini ni sekta ambayo inahitaji ushirikiano, mfano wafugaji wanaposafirisha mifugo kutoka eneo moja kwenda jingine kunakuwa na changamoto za kisera ,kisheria hivyo kupitia ushirikiano huu changamoto nyingi tunaweza kuzimaliza kwa ustawi wa pande zote mbili,’’ alisema Dkt. Omary

Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina akifungua kikao cha ushirikiano baina ya Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ) upande wa Sekta ya Mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jiji Mtumba Mkoani  Dodoma, Machi 03,2023.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya kilimo, umwagiliaji, maliasili na Mifugo Zanzibar, Dkt. Omary Ali Amir akiongea na wajumbe wakati wa kikao cha ushirikiano baina ya  Serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya jamhuru ya muungano wa Tanzania (SMT) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jiji Mkoani Dodoma, Machi 03, 2023.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Venance Ntiyalundura akiongea kwenye kikao cha ushirikiano baina ya  Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya jamhuru ya muungano wa Tanzania (SMT) kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina (wa tatu kutoka kulia) kufungua kikao hicho  kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jiji Mtumba Mkoani Dodoma Machi 03,2023.

Sehemu ya washiriki wa kikao cha ushirikiano baina ya  Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ) Sekta ya mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jiji Mtumba Mkoani Dodoma Machi 03,2023.

Kaimu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (wa Tano kutoka kulia ) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe walioshiriki  kikao cha ushirikiano baina ya Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwenye Sekta ya mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jiji Mtumba Mkoani  Dodoma, Machi 03,2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni