Nav bar

Ijumaa, 29 Julai 2022

SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA WANAWAKE SEKTA YA UVUVI

Serikali imesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia rasilimali za uvuvi na wamekuwa wadau wakubwa katika kuhakikisha kuwa, biashara ya mazao ya uvuvi inaimarika ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia suala la udhibiti ubora wa Mazao ya uvuvi na masoko, Bw. Steven Lukanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah wakati akizindua mtandao wa wanawake, wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya Ziwa Tanganyika ambapo amewataka wanawake kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwa na sauti moja itakayowasaidia katika kutatua changato mbalimbali, Julai 27,2022 Mkoani Kigoma.
Alisema mchango huo wa wanawake unastahili kupewa thamani kubwa hasa katika kuweka mikakati ya kusimamia changamoto zao ikiwemo kuanzisha Dawati la Jinsia la Uvuvi Wizarani ili shughuli za masuala ya wanawake ziweze kuratibiwa.
“ninatambua kuwa wanawake wamejiunga katika vikundi mbalimbali ambavyo vinarahisisha utendaji wa shughuli zao za uvuvi na shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani, pamoja na hayo vikundi hivi vinakabiliwa na changamoto kama upatikanaji wa masoko, taarifa mbalimbali za bei ambapo shughuli zao zina kuwa ngumu ” alisema Bw. Lukanga
Aidha alisema Wizara imeweka juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali za wadau wa Sekta ya Uvuvi ili kuongeza mchango wa Sekta kwenye uchumi wa nchi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara za mazao ya uvuvi, kuzuia uvuvi haramu, kuzuia utoroshwaji holela wa rasilimali za uvuvi, na kuwezesha uvuvi endelevu.
Aliongeza kuwa Juhudi hizi zinalenga kuwezesha wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi ambao 50% ni wanawake ili waweze kuhimili ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi na kuwashukuru shirika la FAO kupitia Mradi wa Fish4ACP unaotekeleza mradi na kuimarisha Mnyororo wa thamani katika Ziwa Tanganyika.
“Juhudi hizo zote, zinalenga kuwaunganisha wanawake wa Tanzania nzima, kupitia vikundi vyao Ili kuwa na sauti ya pamoja, kubadilishana mawazo na uzoefu katika kupata uhakika wa masoko kupitia mtandao huu pamoja na mambo mengine.”
Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia uendelezaji wa rasilimali za uvuvi Bi. Merisia Palazo alisema wanawake wote wanaojishughulisha katika mnyororo wa Uvuvi wanatambulika na ndio maana kukawa na jukwaa linalowawezesha kuelezea mambo yao mbalibali yanayowakabili.
Aidha Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka Shirika la chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (FAO), Bi. Oliva Mkumbo alisema lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia uvuvi ili kuinua kipato cha familia na kuondokana na umasikini.
Aliongeza kuwa kutokana na mchango mkubwa wa kina mama katika shughuli za kiuchumi mradi huo unalenga kumgusa kila mwanamke huku akisema kama shirika litaendelea kufungua matawi katika maeneo mbalimbali na hatimaye sekta ya uvuvi kuwa yenye tija.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Kitaifa Beatrice Mmbaga alieleza kuwa kuzinduliwa kwa jukwaa hilo ni sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili kina mama katika nyanja ya uvuvi.


Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa kinachoratibu Muongozo wa Kuendeleza Uvuvi Mdogo nchini, Bw. Yahaya Mgawe ( wa pili kulia) akieleza jambo alipotembelea na kuona kazi zinazofanyika katika Mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma, Julai 28, 2022


Baadhi ya wanachama wa Mtandao wa Wanawake wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA) wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wao mara baada ya kutembelea Mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma kujionea shughuli zinazofanyika katika Mwalo huo, Julai 28, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni