Serikali imesema itawachukulia hatua kali ikiwemo kuwafutia leseni wachunaji wa ngozi katika machinjio ya Manispaa ya Morogoro wanaotoboa ngozi za mifugo na kuifanya kukosa thamani licha ya kupatiwa mafunzo na vitendea kazi.
Akizungumza (15.3.2021) mara baada ya
kufanya ziara ya kukagua uzalishaji wa ngozi bora zinazohitajika katika soko,
Kaimu Mkurugenzi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel
Bura alisema licha ya kufanyika mafuzo ya uchunaji bora wa ngozi lakini bado
wapo watu wanaokiuka taratibu zilizowekwa.
Alisema mafunzo yaliyotolewa yamesaidia
kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ngozi bora lakini Serikali haitawafumbia macho
baadhi ya wachunaji wa ngozi wanaoendelea kutoboa ngozi kutokana na mahitaji
makubwa yaliyopo hasa katika viwanda vikubwa vya ngozi vilivyoanzishwa.
“Tulizitoa lesei hizi kwa sheria ya
ngozi namba 18 ya mwaka 2008, lakini pia tulitoa mafunzo ya uchunaji wa ngozi
ili kuzipa thamani ngozi mnazozalisha lakini kuna baadhi yenu bado wanafanya
makosa kwa kutoboa ngozi, sasa makosa haya yakijirudia tutawafutia leseni”
alisema Bura
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya
tano chini ya Rais Dkt John Magufuli imejidhatiti kwa kuanzisha na kufufua
viwanda nchini ikiwemo kiwanda cha ngozi cha ACE Leather cha Morogoro na kiwanda
cha ngozi kilichopo Moshi, hivyo kitendo cha kuendelea kutoboa ngozi hizo ni
kurudisha nyuma jitihada za Serikali.
Aidha, aliwataka wachunaji hao
kuhakikisha wanaendelea kuzingatia sheria katika utendaji wa kazi zao sambamba
na kutengeneza upya leseni zao ambazo zipo ukingoni kuisha muda wake wa kipindi
cha mwaka mmoja ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
Mkaguzi mkuu wa nyama Bw. Joseph Kupa
wa Manispaa ya Morogoro amesema kuwa
pamoja na mambo mengine wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watu kushindwa
kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria sambamba na magonjwa ya
ngozi.
Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni
pamoja na baadhi ya wafugaji kuendelea kupiga chapa mifugo yao jambo
linalosabisha ngozi kukosa thamani huku magojwa kama Exiima na Lab Skin ambayo
kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakishambulia mifugo.
“Changamoto tunazopata mara nyingi ni
mifugo inakuja hapa ikiwa imepigwa chapa na mingine imeshambuliwa na magonjwa
ya ngozi sasa ikifika hapa inakuwa tayari haina thamani hata hatuwezi kuichuna
kwa sababu haiwezi kununuliwa na inatokana na baadhi ya wafugaji kutokuwa na
elimu yakutosha juu ya umuhimu wa ngozi” alisema Kupa
Kwa upande wake mwenyekiti wa wachunaji
wa ngozi katika machinjio ya manispaa ya Morogoro, Mapinduzi Ernest ameishukuru
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa elimu waliyowapa ambayo inawasaidia kwa kiasi
kikubwa kuzalisha ngozi bora na kuiomba Serikali kufikisha elimu kwa wafugaji
juu ya upigaji chapa ili kupata ngozi bora.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura (katikati) akiangalia Ngozi kwenye kiwanda cha ACE Limited kilichopo mkoani Morogoro wakati wa ziara yao mkoani humo. Kulia ni Afisa Mifugo kutoka WMUV, Bi. Mariam Muchakila na kushoto ni Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Ngozi cha ACE Limited, Bw. George Obol. (15.03.2021)
Mkaguzi wa Ngozi kutoka
kiwanda cha Ngozi cha ACE Limited, Bw. Godson Shayla (wa tatu kutoka kushoto)
akitoa maelezo kwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo Usalama wa
Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura(wa nne kutoka kushoto) ya namna
ya kuchuna Ngozi na jinsi walivyopanga kutoa adhabu kwa yoyote atakayetoboa
Ngozi wakati wa kuchuna Ngozi hizo kwenye Machinjio ya Manispaa ya Morogoro.
(15.03.2021)
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi
wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura (
wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Machinjio ya
Manispaa ya morogoro na wachunaji wa ngozi za Mifugo mara baada ya kukagua
namna yanavyofanya uchunaji kwa kuzingatia sheria na kanuni katika Machinjio
Iyo mkoani Morogoro. (15.03.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni