Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali imeweka lengo la kuhakikisha Sekta ya
Uvuvi kupitia ufugaji samaki inazalisha idadi kubwa ya samaki sambamba na
samaki wapatikanao kwenye maji ya asili.
Akizungumza jana
(10.03.2021) alipokuwa akikagua shughuli zinazofanywa na Kituo cha Ukuzaji
Viumbe Maji cha Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, Waziri Ndaki amesema
tasnia ya ufugaji samaki imekuwa na mwitikio mkubwa kwa sasa kutokana na
mahitaji ya soko la samaki kuongezeka hivyo jitihada nyingi zinafanyika
kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki.
“Kwa sasa tasnia ya ufugaji
samaki imekuwa ikitoa faida kubwa kwa wanaojishulisha na ufugaji hivyo natoa
wito kwa watu kujitokeza kwa wingi kufuga samaki na pia na toa wito kwa vituo vyetu vya
ukuzaji viumbe maji vilivyopo nchini kuhakikisha vinaongeza uzalishaji wa
samaki kwa kuwa mahitaji ya vifaranga ni mengi.” Amesema Mhe. Ndaki
Aidha, amesema Wizara ya
Mifugo na Uvuvi itahakikisha inaendelea kuviboresha vituo hivyo kwa kuboresha
miundombinu ya uzalishaji vifaranga na kupanua uwezo wake ili viweze kwenda
sambamba na mahitaji ya vifaranga kwa watu wanaofuga samaki.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael
Madalla amesema wizara ipo katika hatua mbalimbali ya kupata programu maalum ya
simu ya mkononi itakayoweza kutumiwa na watu wanaotaka kufahamu mambo
mbalimbali kuhusu ufugaji samaki na namna ya kupata vifaranga vya samaki kutoka
katika vituo ambavyo vipo chini ya wizara.
Pia, Dkt. Madalla
amemfahamisha Waziri Ndaki uboreshaji ambao unafanyika katika Kituo cha Ukuzaji
Viumbe Maji cha Kingolwira kwa kupanua shughuli za uzalishaji wa vifaranga vya
samaki aina ya sato na pia kituo kipo mbioni kuanza uzalishaji wa vifaranga vya
samaki aina kambale.
Kuhusu bei ya vifaranga vya
samaki amesema kwa sasa vituo vya ukuzaji viumbe maji vilivyo chini ya Wizara
ya Mifugo na Uvuvi vinauza kifaranga kimoja cha samaki aina ya sangara kwa
Shilingi 100 na vimekuwa vikiwarahisishia wahitaji wa vifaranga kuwafikishia
popote walipo bila ya ulazima wa wao kufika katika vituo hivyo.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Vumbe Maji Kingolwira Bw. Hamady Makorwa amesema mikakati ya kituo katika kuendeleza shughuli za uzalishaji ni kufikia uzalishaji wa vifaranga 600,000 kwa mwezi hivyo kituo kinahitaji mabwawa yasiyopungua 26 na sato wazazi wasiopungua 24,000 ambapo kwa sasa wapo 5,430.
Amefafanua kwa sasa
vifaranga vya samaki vilivyopo katika kituo hicho ni 38,000 huku tayari
wamepokea maombi ya vifaranga zaidi ya 180,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki amefika kwa mara ya kwanza katika Kituo cha Uzalishaji
Viumbe Maji cha Kingolwira lengo likiwa ni kuhakikisha tasnia ya ufugaji samaki
inakuwa kwa uwepo wa idadi kubwa ya upatikanaji wa vifaranga vya samaki nchini
vitakavyouzwa kwa bei nafuu zaidi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla juu ya vifaranga ambavyo viko tayari kusafirishwa kwa wahitaji ambavyo vinahifadhiwa katika matanki. Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (10.03.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akiangalia vifaranga vya samaki aina ya sato ambavyo
vimezalishwa na Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani
Morogoro, na viko tayari kwa ajili ya kusafirishwa na kuwekwa kwenye mabwawa
ili kuendelea kukuzwa na hatimaye kufikia ukubwa wa samaki unaotakiwa sokoni.
(10.03.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati), akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla (wa kwanza kulia) na Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Vumbe Maji Kingolwira Bw. Hamady Makorwa (wa kwanza kushoto), wakati Waziri Ndaki akipatiwa maelezo ya namna vifaranga vya samaki vinavyozalishwa katika kituo hicho kilichopo Mkoani Morogoro. (10.03.2021)
Mkurugenzi wa Idara ya
Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla
akizungumza wakati wa ugeni wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na
baadhi ya wafanyakazi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira (hawapo
pichani). (10.03.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) wakijadiliana jambo na Mkurugenzi wa
Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla,
wakati Waziri Ndaki alipokuwa akikagua maboresho ya miundombinu ya uzalishaji
vifaranga vya samaki katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo
Mkoani Morogoro. (10.03.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Kituo cha Ukuzaji
Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, mara baada ya kufanya ziara
ya kikazi ya siku moja katika kituo hicho na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na
kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki kulingana na mahitaji ya soko.
(10.03.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa
Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla
(anayemfuata), namna samaki wazazi aina ya sato wanavyozalisha mayai na njia
wanazotumia wataalamu kutoka mayai hayo kwenye midomo ya samaki na kuyaweka
katika hatua mbalimbali ili kupata vifaranga. Waziri Ndaki amefanya ziara ya
kikazi ya siku moja katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo
Mkoani Morogoro. (10.03.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni