Na. Edward Kondela
Serikali imesema katika bajeti ya mwaka
wa fedha 2021/22 ina mpango wa kuanzisha vituo vya ukuzaji viumbe maji katika
halmashauri 80 za wilaya ikiwa na lengo la kuhakikisha kila halmashauri inakuwa
na kituo hicho ambacho kitatumika kama shamba darasa kwa ajili ya kufundisha
wananchi namna ya kufuga samaki.
Akizungumza jana (17.03.2021) wakati
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kituo cha
ukuzaji viumbe maji kinachozalisha vifaranga vya samaki cha Kingolwira
kilichopo Mkoani Morogoro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
amesema mkakati wa serikali kupitia vituo hivyo vitakavyokuwepo katika
halshamauri zote za wilaya ni kuwa na samaki wengi wafugwao kwa njia mbalimbali
ikiwemo ya mabwawa na kufikia uzalishaji wa samaki wa asilimia 50 kwa njia ya
kufuga na asilimia 50 wanaotokana na maji ya asili.
“Kupitia tasnia hii ya ukuzaji viumbe
maji tunataka kuweka nguvu kubwa ili tuweze kuvuna rasilimali ya uvuvi iweze
kusaidia lishe, ajira na kuondoa umasikini kwa wananchi, hivyo wizara inaweka
mikakati ya kuhakikisha inafikia malengo yake kupitia tasnia hii.” Amesema Mhe.
Ndaki
Aidha, Waziri Ndaki amesema Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ina mpango wa kuhakikisha inavipa uwezo mkubwa na kuvikarabati
vituo vyote vya ukuzaji viumbe maji vilivyopo nchini ili viweze kwenda sawa na
uzalishaji wa vifaranga vya samaki kulingana na mahitaji yake.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu wa
Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ameipongeza Wizara
ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka jitihada mbalimbali za kuhakikisha inazalisha kwa
wingi vifaranga vya samaki pamoja na kutoa elimu juu ya ufugaji wa samaki.
Amesema kamati hiyo itaangalia vyema
bajeti ya wizara itakayowasilishwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2021/22 ili
iweze kuwa na tija na kuleta matokeo chanya hususan katika tasnia ya ufugaji
samaki kwa kuwa bado ni eneo jipya ambalo watu wengi wanahitaji kujifunza na
kujiingiza katika ufugaji huo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.
Imani Kapinga amesema kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani
Morogoro, katika kutekeleza majukumu yake kati ya mwaka 2010 hadi 2020 kimetoa
mafunzo kwa wananchi 11,280 kutoka mikoa mbalimbali pamoja na kuzalisha vifaranga
vya samaki aina ya sato zaidi ya milioni sita vilivyosambazwa maeneo mbalimbali
nchini.
Katika ziara hiyo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuhakikisha inakiboresha kituo cha Kingolwira kwa kufanya upanuzi wa baadhi ya majengo kwa ajili ya ukuzaji viumbe maji na kuiomba wizara izidi kufanya maboresho zaidi katika maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kufuatia ushauri mbalimbali uliotolewa na wajumbe hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni