Nav bar

Alhamisi, 19 Aprili 2018

WANAOAGIZA NYAMA, MAZIWA NA SAMAKI KUTOKA NJE YA NCHI SIKU ZAO ZAHESABIKA - ULEGA KIGOMA


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega, amesema kuwa wanaoagiza nyama, maziwa na samaki kutoka nje ya nchi, siku zao zahesabika kutokana na nchi kuwa na mifugo ya kutosha kama vile Ngombe, Mbuzi, Kondoo, Kuku na Punda. Hivyo, Taifa kama Tanzania halina sababu yoyote ya kuagiza mazao hayo ya mifugo na uvuvi kutoka nje ya nchi.
Naibu waziri Ulega aliyasema hayo alipokuwa katika ziara ya siku tatu Mkoani Kigoma ya kutembelea Mwalo wa Samaki wa Muyobozi Uliyopo Wilayani Uvinza na Mwalo wa Kibirizi na kituo cha Taasisi ya Tafiti za Uvuvi Tanzania TAFIRI Kigoma.
“Sioni kwanini tuagize nyama na maziwa  toka nje  ya nchi, hatuwezi kuendelea kuangiza nyama, maziwa na hata mazao ya uvuvi, kwa nini tusiwekeze katika rasilimali zetu za ndani  katika mifugo na samaki na kuongeza pato la taifa? “Aliuliza Ulega.
Ulega  aliongeza kwa kusema kuwa Wizara yake haitawavumilia  wafanyabiashara wanaoagiza nyama, maziwa na mazao ya samaki  toka nje ya nchi kwani sekta ya mifugo na uvuvi ni sekta ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuleta tija katika taifa.
Tarkibani “tani elfu 20 za samaki zinaingizwa kutoka nje ya nchi kila mwaka, samaki ambao wanafugwa katika maeneo mengine duniani, lakini sisi hapa nchini tunao katika mazingira ya asili.” Alisema
 Na hapa Mhe. Ulega aliitaka TAFIRI kuhakikisha wanawafikia wafugaji wa samaki kwa kufanya tafiti zao ili kujua changamoto wanazokutana nazo na kujua namna ya kuzitatua, akitolea mfano wa chakula sahihi kinachotakiwa kupewa masamki wanaofugwa na kuangalia miundombinu ya kufugia.
Akizungumzia suala la zana za uvuvi katika ziwa Tanganyika alipokuwa akiongea na watafiti na watumishi wa TAFIRI, Ulega alisema “TAFIRI mfanye tafiti ya aina ya nyavu zinazotumiwa kwa kiasi kikubwa na wavuvi  ili kuona kama zinafaa kuendelea kutumika, maana kumekuwa na malalamiko toka kwa wavuvi yanayopelekea kushuka kwa kiwango cha upatikanaji wa samaki na dagaa katika ziwa hili kutokana na matumizi ya nyavu hizo.” Alisema
Sambamba na hilo Ulega alisema Wizara yake ina mpango wa kuimarisha eneo la tafiti kwa kuongeza rasilimali fedha kwa kukarabati miundombinu na kuongeza rasilimali watu.
“Kila Mwaka TAFIRI itakuwa inafanya tafiti kuhusu mambo ambayo Wizara itakuwa imeyaelekeza ili kuondokana na suala la watafiti hawa kufanya kazi za watu wengine.” Alisema
Akizungumzia swala la mafanikio ya soko la nyama la nje ya nchi, Ulega alisema, “Hatuwezi kusafirisha nyama nje ya nchi kama mkakati wetu wa chanjo ya mifugo hauko sawa, lazima tuwe na mkakati wa kudhibiti magonjwa ya mifugo, soko la kimataifa linaangalia sana swala hili, Sisi kama Wizara tunaenda kusema kuwa kwa yoyote anayetaka kufuga swala la chanjo ni lazima.” Alisisiza Ulega.
Ulega aliendelea kusema kuwa ni lazima wizara kutengeneza mikakati ambayo itamfanya mfugaji asitaabike wazo wambalo amesema kama litaridhiwa litafanyiwa kazi.
“kuna watu wanaona mifugo ni balaa, mifugo siyo balaa mifugo ni neema.” Alisisitiza.
Aidha Ulega alisisitiza suala la uwekezaji kwa ufugaji wa samaki kama njia ya kusaidia kupunguza kiwango kikubwa cha uvuvi haramu wa samaki katika maeneo mbalimbali nchini, huku akipongeza jitihada za taasisi ya utafiti wa samaki TAFIRI kushirikiana na wananchi na kuonesha mfano wa namna ya ufugaji bora wa samaki unaowaonesha wafugaji wa samaki kuitumia ili kufikia malengo waliyokusudia.
Naibu Waziri Ulega pia alisema Serikali imepanga kuongeza makusanyo katika sekta ya mifugo kutoka bilioni kumi na sita hadi bilioni hamsini baada ya kuifanya mifugo ya ndani kuwa bora na kuwa ya kiushindani katika soko la kimataifa, hivyo suala la chanjo litakuwa la lazima.
Kulia Dkt. Emmanuel Sweke Kaimu Mkurugenzi wa kituo wa kituo cha  Taasisi ya Utafiti wa  Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kigoma,  akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega aliyekaa katikati  wakiwa katika boat wakielekea kuangalia kizimba cha kufugia samaki katika maji ya ziwa Tanganyika, kushoto ni Afisa Mifugo wa Mkoa wa Kigoma Bw. Noel Byamungu.

Kushoto Dkt. Emmanuel Sweke, Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha  Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kigoma akimuonyesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega katikati, kizimba cha kufugia samaki kilichopo katika maji ya ziwa Tanganyika hakipo pichani, alipotembelea kituo hicho mjini kigoma jana. Kulia ni Afisa Mifugo wa Mkoa Bw. Noel Byamungu.

Aliyesimama ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega, akiongea na watumishi wa kituo cha  Taasisi ya Utafiti wa  Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kigoma, pamoja na watafiti hawapo pichani, alipotembelea kituo hicho, kulia ni Dkt Emmanuel Sweke, Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, na kushoto ni  Mkurugenzi wa tafiti na mafunzo katika chuo cha mafunzo ya uvuvi  FETA Kigoma, Bw. Simtie Ambakisye.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni