WANUFAIKA TASFAM BAGAMOYO WAJENGEWA UELEWA WA MRADI
Wanufaika wa Mradi wa Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (TASFAM) Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Machi 27,2026 wamejengewa uelewa kuhusu maeneo watakayonufaika kupitia mradi huo.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa kueleweshwa maeneo mbalimbali yatakayoguswa na mradi huo, Wanufaika hao wameishukuru Serikali kwa kuwapa fursa hiyo ya miaka 5 itakayowawezesha kuboresha shughuli zao za uvuvi na ukuzaji viumbe maji.
“Tunaomba wataalam kupitia mradi huu msikae ofisini mje huku uwandani ili muone kwa vitendo namna tunavyofanya shughuli zetu ili kwa pamoja tuweze kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huu” Amesema Bw. Machano Ally muasisi wa chama cha Ushirika cha uzalishaji zao la Mwani cha Msichoke.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha uzalishaji zao la mwani cha “Nasi Tumo” Bw. Rashid Gubi ameiomba Serikali kupitia mradi huo kuwasaidia boti za kisasa zitakazowasaidia kutekeleza shughuli zao kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kuhamisha maeneo yao ya kilimo cha zao hilo pindi wanapolazimika kufanya hivyo.
Awali akizungumza wakati wa kuutambulisha mradi huo kwa wavuvi na wakuzaji viumbe maji waliopo Wilaya ya Bagamoyo, Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Fredrick Musa amesema kuwa hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi huo inajumuisha kusikiliza matakwa na maoni ya wanufaika hao na kuwapa elimu itakayowasaidia kufanya shughuli zao kwa ufanisi.




Maoni
Chapisha Maoni