WAFUGAJI NG'OMBE WA MAZIWA WAPEWA ELIMU YA NADHARIA NA VITENDO KUONGEZA UZALISHAJI NCHINI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeendelea kutoa Mafunzo ya nadharia na vitendo kwa wafugaji wa ng’ombe wa Maziwa ili kukuza Tasnia ya Maziwa kwa kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Aprili 13, 2026 Jijini Tanga katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji wa ng'ombe Bora wa Maziwa kupitia Mradi wa Maziwa Faida, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini na kuweza kuwafikia wafugaji 3,000 ndani ya miaka Mitano (5) ya utekelezaji wa Mradi huo, ambapo hadi sasa wafugaji 1,888 wamefikiwa.

"Uboreshaji wa uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa mlionao utasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa bora na hivyo kuongeza kipato katika kaya zenu, na ongezeko la maziwa pia litasaidia kuongeza upatikanaji wa mali ghafi kwa ajili ya kuviwezesha viwanda vya kusindika maziwa, hasa kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho kwa mujibu wa taarifa zilizopo bado kinapata maziwa kidogo ya kusindika kutoka kwa wafugaji walioko mkoani Tanga na mikoa mingine jirani." amesema Ndg. Mdachi

Aidha, Ndg. Mdachi amebainisha kuwa ili ufugaji hapa nchini uwe na tija na endelevu, ni vizuri kushirikisha kwa karibu na kundi kubwa la vijana na wanawake ambao ndiyo wengi na nguzo kuu ya uchumi katika kuimarisha mifumo endelevu ya usalama wa chakula na lishe hapa nchini, barani Afrika na Dunia nzima. 

Vilevile, Ndg. Mdachi amewapongeza Taasisi za LITA na TALIRI kwa namna wanavyoendelea kushirikiana katika kutoa huduma za mafunzo na ushauri elekezi kwa wafugaji na wadau wengine katika Sekta ya mifugo hapa nchini, na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo katika kutoa elimu hiyo katika vituo vingine vilivyoko katika mikoa mingine hapa nchini.

Ndg. Mdachi, amewataka Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kutumia vizuri fursa hiyo adimu na adhimu ya kuwezeshwa kupata mafunzo kama hayo kwa msaada mkubwa kutoka nchi ya Ireland kupitia Taasisi za Utafiti na Mafunzo TEAGASC pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, ambayo yanatolewa bila gharama yoyote ambapo wakati mwingine wangelazimika kulipia na wawe tayari kubadilika na kuboresha ufugaji wao na kuwa wenye tija na endelevu.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Lazaro Mwambene amesema kuwa mafunzo ya hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mpango wa utoaji wa mafunzo kwa wafugaji 3,000 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Muheza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, tangu kuanza kwa utekelezaji wa mafunzo hayo mwishoni mwa mwaka 2022, ambapo LITA imewafikia washiriki 1,888, na kati yao wafugaji ni 1,858 na maafisa ugani 30 na katika awamu hii ya saba ya mafunzo haya yatawafikia wafugaji 310 wakiwemo washiriki 78 na Mafunzo hayo yamekuwa yakianza kwa kupokea changamoto zinazowakabili wafugaji ambapo ufumbuzi wa changamoto zao hujadiliwa kwa pamoja na kufundishwa kwa njia rahisi ya nadharia na vitendo.

Pia, Dkt. Mwambene amesema wafugaji watajifunza maeneo yote muhimu yanayogusa ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa, ikiwemo pamoja na matumizi ya mabanda bora, chakula na lishe bora; uzalishaji, utunzaji, uvunaji, ulishaji na hifadhi ya malisho; utunzaji wa makundi mbalimbali ya ng’ombe wa maziwa, utunzaji wa kumbukumbu, afya (kinga na tiba dhidi ya magonjwa), usindikaji/uongezaji thamani wa mazao ya mifugo ili kuwa na ufugaji wa ng’ombe wenye tija.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba amesema ongezeko la uzalishaji hasa wa maziwa utasaidia kuwa na uhakika wa chakula na lishe, kuongeza kipato katika kaya na Taifa na ongezeko la upatikanaji wa maziwa ghafi yanayohitajika na viwanda vyetu vya ndani vya kusindika maziwa na hivyo kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana na wanawake. 

Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya Muheza, Bw. Abdallah Francis ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi zake za LITA na TALIRI kwa kuongeza jitihada katika kuwafikia wafugaji wa Muheza kwa kuwapatia Mafunzo ambayo yataleta tija kwa wafugaji wa Wilaya hiyo.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi, akihutubia wafugaji wa ng'ombe Bora wa Maziwa, katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji hao kupitia Mradi wa Maziwa Faida, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Buhuri, Aprili 13, 2026 Tanga.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Lazaro Mwambene, akielezea malengo ya Semina, katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji wa ng'ombe wa Maziwa kupitia Mradi wa Maziwa Faida, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Buhuri, Aprili 13, 2026 Tanga.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba, akizungumza na wafugaji wa ng'ombe wa maziwa, katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji wa ng'ombe wa Maziwa kupitia Mradi wa Maziwa Faida, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Buhuri, Aprili 13, 2026 Tanga.

Mfugaji wa ng'ombe wa Maziwa kutoka Wilaya ya Muheza, Bw. Sufiyani Jumanne akielezea changamoto zinazowakumba Wafugaji wa ng'ombe wa Maziwa na namna wanavyopata malisho, katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji hao kupitia Mradi wa Maziwa Faida, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Buhuri, Aprili 13, 2026 Tanga.

Picha ni baadhi ya Wafugaji wa ng'ombe wa Maziwa na wadau wa Tasnia hiyo, wakimsikiliza Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE), Bw. Samwel Mdachi (hayupo picha) alipokuwa akizungumza nao, katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji hao kupitia Mradi wa Maziwa Faida, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Buhuri, Aprili 13, 2026 Tanga.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi (wa saba kulia), akiwa kwenye picha ya pamoja na wafugaji wa ng'ombe wa Maziwa na wadau wa Tasnia hiyo, katika Ufunguzi wa Semina ya Wafugaji hao kupitia Mradi wa Maziwa Faida, iliyofanyika katika Ukumbi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) Buhuri, Aprili 13, 2026 Tanga.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO