SERIKALI KUIMARISHA TASNIA YA KUKU NCHINI
Na. Stanley Brayton
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepania kuimarisha Tasnia ya kuku kwa kushirikiana na wadau wa Tasnia hiyo katika kuleta mabadiliko yenye tija ili kuongeza uzalishaji nchini ambao utasaidia kuinua vipato vya wananchi na Taifa kiujumla.
Akizungumza leo Aprili 11, 2026 Jijini Dodoma katika Kikao cha Mkakati na Viongozi pamoja na wadau wa Mnyororo wa thamani wa kuku nchini, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Uzalishaji kuku ni miongoni mwa Sekta zinazotakiwa kupewa kipaumbele kwani ndio inagusa maisha ya kila mwananchi, na ndipo chakula chenye usalama kinapopatikana, na ni vyema kufanya mabadiliko katika Sekta hiyo ili iwe rasmi na kufuga kisasa kwa kuendana na Teknolojia mpya ya ufugaji kuku.
"Ili kunyanyua Uchumi wetu ni lazima kutanua wigo wa Sekta ya Mifugo katika Tasnia ya kuku kwa kutumia teknolojia mbalimbali, mana tunaweza zalisha kwa wingi mazao ya kuku na kwa ubora zaidi na kuuza nchi za nje na kupata fedha za kigeni pamoja na kukuza mashirikiano ya Kidiplomasia baina ya nchi yetu na nchi zingine." amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru
Aidha, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema ana uhakika kuwa Sekta ya Mifugo katika Tasnia ya kuku inaweza kuwa na Mkakati Mkubwa wa kiuzalishaji Mazao hayo na kuikuza Sekta hiyo ili kuwahudumia wananchi wengi, na ndio mana Wizara ipo katika Mapitio ya Sera za Mifugo ili kiziboresha na kuhakikisha zinaendana na Dira ya Taifa ya 2050.
Vilevile, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa Serikali inawapongeza wazalishaji wote wa chakula nchini ikiwemo wafugaji kuku, na amebainisha kuwa Serikali ipo katika kuhakikisha kuna usalama wa chakula nchi na ndio mana inawaleta wadau wote wa Tasnia ya kuku karibu ili kujua changamoto zao na kuzitatua kwa haraka.
Pia, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amewataka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kujenga Maabara ya kupima vyakula vya Mifugo ili kuwezesha usalama wa chakula cha Mifugo na Wataalam na Wizara na Taasisi za Serikali kuendelea kukutana na wadau mbalimbali wa Tasnia ya kuku na kusaidiana nao katika kukuza Sekta ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amesema tasnia ya kuku ni sehemu muhimu sana katika Sekta ya Mifugo hapa nchini na ndio mana Serikali inasimama kwa ukamilifu katika kuhakikisha Tasnia hiyo inakuwa kwa kasi na kuwanufaisha wananchi kuanzia kwenye chakula hadi kwenye kipato.
Bi. Meena amesema kikao cha leo kitasaidia sana katika kutatua changamoto za kuku na wafugaji ili waweze kufuga kwa urahisi na kupata chakula cha kuku kiurahisi na kwa bei nafuu.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Chama cha Kuku cha Tanzania (PAT), Bw. Costa Mrema ameelezea changamoto mbalimbali zinazowakumba wafugaji wa kuku, ikiwemo gharama kubwa ya Chakula cha kuku, changamoto ya uingizaji kinyemela wa vifaranga vya kuku, uhaba wa Wataalam kwenye Hachari na Mashamba ya kuku, Uwezeshaji wa wafugaji wa kuku kiuchumi, Takwimu na Masoko yake.
Bw. Mrema ameiomba Wizara kuwasaidia wafugaji wa kuku katika kutatua changamoto hizo ambazo zimekuwa ni changamoto zao za kudumu kwa wafugaji hao.





Maoni
Chapisha Maoni