MABALOZI WATEULE WAHIMIZWA KUZINADI FURSA ZA MIFUGO NA UVUVI KIMATAIFA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekutana na Mabalozi Wateule wa Tanzania kwa lengo la kuwafahamisha fursa zilizopo katika sekta za mifugo na uvuvi ili kwenda kuzinadi kwenye Nchi walizopangiwa kuiwakilisha Tanzania  ikiwa ni sehemu ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kimataifa.

Mhe. Dkt. Bashiru amekutana na Mabalozi hao katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma leo Aprili 13, 2026 na kuwaeleza kuwa sekta za mifugo na uvuvi zinahitaji kupanua wigo wa masoko ya kimataifa yatakayochochea uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa wananchi.

“Kama ambavyo mtakavyokuwa  makini na sekta zingine za kiuchumi kama maliasili na utalii, pia sekta za mifugo na uvuvi ni eneo muhimu, nchi yetu bado tuna nafasi ya kujikomboa kiuchumi kutokana na Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kwa hiyo uwakilishi wenu unakuwa na mchango mkubwa katika diplomasia ya uchumi” alisema Mhe. Dkt. Bashiru.

Aidha, Mhe. Dkt. Bashiru ameongeza kuwa Wizara bado inahitaji mashirikiano na mataifa mengine katika maeneo ya teknolojia na miundombinu ya uzalishaji, mitaji, uwekezaji katika uzalishaji wa vyakula vya mifugo na samaki, afya ya mifugo, kuimarisha mbari (mbegu bora) za mifugo, masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na mafunzo na utaalam katika sekta hizo, mambo ambayo yatavutia uwekezaji.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania Nchini Saudi Arabia Mhe. Eng. Zena Ahmed Saidi akizungumza katika kikao hicho ameiomba serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kushirikiana kwa karibu na balozi hizo ikiwa ni pamoja na kuwapatia vielelezo vyote vinavyohusiana na sekta ya mifugo na uvuvi ili kupata nguvu ya kuzitangaza sekta hizo kwa wawekezaji wa kimataifa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa(Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mabalozi Wateule wa Tanzania baada ya kufanya mazungumzo ya kuzitangaza fursa za sekta za Mifugo na Uvuvi yaliyofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma leo Aprili 13, 2026. Wengine ni Naibu Waziri Mhe. Ng’wasi Kamani, Katibu Mkuu Bi. Agnes Meena na Naibu Katibu Mkuu (Mifugo) Dkt. Fabian Madele.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Wasita kulia) akizungumza na Mabalozi Wateule wa Tanzania kuhusu fursa zilizopo kwenye Sekta za Mifugo na Uvuvi wakati wa mazungumzo yaliyofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma leo Aprili 13, 2026.

Balozi wa Tanzania Nchini Saudi Arabia Mhe. Eng. Zena Ahmed Saidi akizungumza wakati wa Kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Mabalozi Wateule kilichofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma 13 Aprili 2026

Mabalozi Wateule wa Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi  wakati wa mazungumzo yaliyofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Mjini Dodoma leo 13 Aprili 2026.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani (kushoto) akichangia jambo wakati wa Mazungumzo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mabalozi Wateule wa Tanzania yaliyofanyika Ofisi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma leo Aprili 13, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO