VITUO 31 VYASITISHWA KUTOA HUDUMA ZA AFYA YA WANYAMA

Na. Stanley Brayton, WMUV

Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) limesitisha Huduma za Vituo 31 vya Huduma za Afya ya Wanyama Mkoani Dar es Salaam, hii ni kutokana na Vituo hivyo kutokuwa na uhalali na kutokidhi vigezo vya kutoa Huduma hizo, ikiwemo kutokuwa na Usajili pamoja na kutozingatia Sheria ya Veterinari SURA 319 ya mwaka 2003.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), wakati wa Ukaguzi wa Vituo mbalimbali vya kutolea Huduma za Afya ya Wanyama pamoja na Wataalam wake, leo Machi 6, 2026 Mkoani Dar es Salaam, Mkaguzi wa Baraza hilo, Dkt. Winston Billy, amesema mpaka sasa wamekagua jumla ya vituo 261 vya Huduma hizo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam na kukuta changamoto kwenye Vituo 31 ambavyo havijakidhi vigezo na kuamua kusitisha Huduma za Vituo hivyo.

"tumesitisha Huduma kwenye Vituo hivi kutokana na wamiliki kutofuata Sheria za Veterinari na tumewaelekeza wamiliki na Wataalam wa Huduma za Afya ya Wanyama kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ili kutoa Huduma Bora kwa Wanyama na wafugaji” amesema Dkt. Billy

Aidha, Dkt. Billy amebainisha kuwa Baraza linataka wafugaji wakienda kwenye Vituo vya Huduma ya Afya ya Wanyama wapate Huduma iliyo Bora na iliyokidhi vigezo na viwango stahiki kutokana na muongozo wa Baraza, na Baraza linaendelea kufanya ukaguzi katika mikoa mingine ili kuhakikisha Huduma hizo zinatolewa kwa ubora na kwa kufuata sheria.

Vilevile, Dkt. Billy amesema lengo la Baraza ni kupita na kukagua pamoja na kuangalia kama yale makubaliano ya awali wakati Kituo kinasajiliwa kama yamefuatwa na yanaendelea kufuatwa na kama mtaalam aliyopo pale kasajiliwa na Baraza.

Pia, Dkt. Billy ametoa rai kwa wamiliki wa Vituo vya Huduma za Afya ya Wanyama na Wataalam ambao wako kwenye Vituo hivyo kuendelea kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo ya Baraza ili kuweza kuwahudumia wafugaji vizuri, na amewataka wafugaji kupata Huduma katika Vituo na Wataalam waliosajiliwa na wenye sifa stahiki wanaotambuliwa na Baraza kwa ajili ya ustawi wa sekta ya mifugo nchini.

Mkaguzi wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dkt. Winston Billy (kushoto), akikagua vyeti vya Usajili wa Wataalam na Kliniki ya Mama Pembejeo Agrovet kama vimesajiliwa kihalali na kuhuishwa na Baraza, wakati wa zoezi la kukagua shughuli za utoaji Huduma za Afya ya Wanyama katika Vituo na Kliniki za Wanyama, Machi 6, 2026 Dar es Salaam.

Mkaguzi wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dkt. Winston Billy (kushoto), akiweka kumbukumbu ya Taarifa ya Kliniki ya ARM Agrovet na Wataalam wake kwenye kitabu cha kumbukumbu, wakati wa zoezi la kukagua shughuli za utoaji Huduma za Afya ya Wanyama katika Vituo na Kliniki za Wanyama, Machi 6, 2026 Dar es Salaam.

Mkaguzi wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dkt. Winston Billy, akikagua dawa za Wanyama kama hazijaisha muda wake pamoja na uhifadhi wa chanjo za wanyama, wakati wa zoezi la kukagua shughuli za utoaji Huduma za Afya ya Wanyama katika Vituo na Kliniki za Wanyama, Machi 6, 2026 Dar es Salaam.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO