UFUGAJI SATO BAHARI (CHOTARA) NA KAA NI FURSA MUHIMU KATIKA MASOKO YA MAZAO YA UVUVI - PROF. SHEIKH

Na. Stanley Brayton

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh amesema teknolojia mpya ya Ukuzaji kaa na Samaki aina ya Sato (Chotara) ni fursa muhimu katika kufungua Masoko ya nje na kukuza Sekta ya Uvuvi.

Akizungumza Prof. Sheikh, alipotembelea shamba la Ukuzaji Viumbemaji la Tanga Fish Aqua, leo Februari 28, 2026 Mkoani Tanga, amesema uvumbuzi wa teknolojia mpya ya Ukuzaji Kaa na Sato ambae anafugika kwenye maji Bahari kwa njia ya Vizimba, ambazo hutumia maboksi ya plasti katika kukuza Viumbemaji hao, imeleta tija kwenye tasnia ya Uvuvi kwa kuongeza Uzalishaji wa zao hilo la Uvuvi nchini.

"Kaa na Sato waweza kukua kwenye maji Bahari, na ni fursa adhim kwa wananchi, kwani inafungua Masoko ndani na nje ya nchi ambapo upelekea kuinua Uchumi wa mtu binafsi na wa Taifa kiujumla.” amesema Prof. Sheikh

Aidha, Prof. Sheikh amebainisha kuwa kilo moja ya kaa ni shilingi 25,000 hadi 30,000 kiasi ambacho kinaweza mpatia mtu utajiri, na Ufugaji huo unawezekana na ni kitu rahisi kwani aihitaji sayansi kubwa sana kwakuwa mabwawa ni ya kawaida na ata Miundombinu yake ni rahisi na ndani ya mwezi mmoja unaweza kuvuna.

Vilevile, Prof. Sheikh amesema watu wengi wana hamu ya kufuga samaki bahari na kaa, na hawajui teknolojia hiyo mpya na  jinsi gani ya kufuga, hivyo ni vyema kuwapa elimu na kuwahamasisha kufanya Ufugaji huo kwa teknolojia ya kisasa.

Pia, Prof. Sheikh ameweka wazi kuwa shamba hilo la Tanga Fish Aqua ni muhimu kwa wafugaji wa Mkoa wa Tanga katika kujifunza namna ya kuweza kufuga kaa na Samaki Bahari ili kuleta tija katika Sekta ya Uvuvi, na Serikali  itaangalia utaratibu wa kurasimisha shamba darasa hilo.

Prof. Sheikh amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya Vijana wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ili waweze kukuza Viumbemaji bila changamoto zozote na kujipatia kipato na amewataka Maafisa na Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa upande wa Sekta ya Uvuvi kuacha kufanya kazi kwa nadharia bali vitendo ili kufanya Mageuzi ya Tasnia hiyo katika Sekta, kwa kuanzia ufugaji  wa samaki wa vizimba vya bahari aina tatu za vifaranga ambao ni Mwatiko, kolekole na Sato-chotara, ambao wataanza kuzalishwa na vituo vilivyopo chini ya Wizara.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh (wa nne kulia), akitazama Teknolojia ya uwekaji chumvi kwenye maji kwa ajili ya kukuzia Sato Bahari, alipotembelea shamba la Ukuzaji Viumbemaji la Tanga Fish Aqua, Februari 28, 2026 Tanga.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh (wa pili kulia), akitoa maelekezo baada ya kukagua Vizimba vya kufugia kaa, alipotembelea shamba la Ukuzaji Viumbemaji la Tanga Fish Aqua, Februari 28, 2026 Tanga.

Wataalam wa kufuga kaa wakiangalia hali ya Viumbe Maji hao kabla ya kuwapa chakula, katika shamba la Ukuzaji Viumbemaji la Tanga Fish Aqua, Februari 28, 2026 Tanga.

Picha ni muonekano wa Vizimba vya kufugia kaa vilivyopo kwenye shamba la Ukuzaji Viumbemaji la Tanga Fish Aqua, Februari 28, 2026 Tanga.

Picha ni muonekano wa Vizimba vya kufugia Sato Bahari vilivyopo kwenye shamba la Ukuzaji Viumbemaji la Tanga Fish Aqua, Februari 28, 2026 Tanga.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO