SERIKALI YAONGEZA NGUVU KWA MAAFISA UGANI
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kuimarisha uwezo wa maafisa ugani wa sekta ya mifugo kwa kuwapatia mafunzo rejea yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wafugaji na kuongeza uzalishaji wa mifugo nchini.
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa siku mbili Kwa upande wa maafisa ugani wa Mifugo yamehitimishwa leo Machi 10, 2026 Katika ukumbi wa IFM Wilayani Chato mkoani Geita kwa kuwahusisha maafisa ugani kutoka Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi.
Akizungumza wakati wa hitimisho la mafunzo hayo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Afisa Mifugo Mkuu, Bi. Mary Yongolo amewashukuru maafisa ugani kwa nidhamu waliyoionesha katika kipindi chote cha mafunzo hayo.
"Hakikisheni maarifa mliyoyapata yawe chachu ya kuboresha utendaji kazi wenu pindi mrejeapo vituoni ili kuleta tija katika sekta ya mifugo." Amesema Bi. Yongolo
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Dkt. Sostenes Nkombe, amewapongeza washiriki kwa ushiriki wao katika mafunzo hayo na kuwataka kuwa mfano kwa maafisa wengine watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.
Aidha, amesema kuwa mafunzo hayo yana mchango mkubwa katika kuimarisha ufanisi wa maafisa ugani katika kuwahudumia wafugaji na kusaidia maendeleo ya sekta ya mifugo katika ngazi za halmashauri.
Kwa upande wake mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Frank Ipugute ambaye ni Afisa Mifugo Halmashauri ya Wilaya ya Chato, ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo hayo na kuomba yaendelee kutolewa mara kwa mara, pia yatolewe katika ngazi za Halmashauri ili yaweze kuwafikia maafisa ugani wengi zaidi na kuboresha huduma kwa wafugaji.





Maoni
Chapisha Maoni