SERIKALI YAKABIDHI BILIONI 7 KWA VIJANA 308 MRADI WA BBT UVUVI

 Serikali kupitia Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhi hundi ya shilingi Bil. 7 kuwezesha mitaji kwa vijana waliohitimu mafunzo ya program ya Jenga Kesho iliyo Bora kwa upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) ambapo zitatumika kwenye shughuli za ukuzaji viumbe maji.

Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi hiyo Mgeni rasmi wa hafla hiyo ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka amesema kuwa fedha hizo zinatolewa kama mikopo yenye mashart nafuu kwa vijana kwa ajili ya kuwezesha mitaji, vifaa, pembejeo muhimu za ukuzaji  viumbe maji pamoja na posho ya kujikimu kwa washiriki.

"Program hii haitaishia tuu hapa , itaenda ukanda wa pwani na mtwara kwani mradi wenyewe una sura ya ukuzaji wa uchumi wa buluu ” Amesema Mhe. Nanauka

Aidha amewakumbusha vijana wanufaika kuwa hii ni mikopo, wana wajibu wa kufanya marejesho kwa uaminifu ili fedha zinazopatikana ziweze kuwasaidia vijana wengine ambao wana uhitaji.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ng'wasi Kamani amesema kuwa uwezeshaji wa vijana hao ni sehemu ya mikakati ya wizara ya kuongeza uzalishaji pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa sambamba na utoaji wa ajira nchini.

"Takwimu zinaonesha kuwa kwa sasa kila mtu anakula samaki kilo 7.9 kiasi ambacho kiko chini ukilinganisha na hitaji la shirika la chakula na Kilimo Duniani (FAO) kinachotaka  kila mtu kula kilo 20 za samaki kwa mwaka hivyo hali hiyo inaonesha fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji kupitia miradi ya ufugaji samaki kwenye vizimba ili kukidhi hitaji la ulaji wa samaki nchini" Ameongeza Mhe. Kamani.

Akizungumza kwa niaba ya katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Agness Meena, Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa program ya jenga kesho iliyobora (BBT Uvuvi) ni mpango unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi sambamba na kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana.

"Fedha hizi zinatarajiwa kuwawezesha mitaji vijana 308 ambapo vijana  160 watatekeleza miradi ya ufugaji samaki kwenye vizimba, vijana148 watatekeleza miradi ya ufugaji jongoo bahari, kilimo cha mwani pamoja na unenepeshaji wa kaa” Amesema Prof. Sheikh.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt Semvua Mzighani ambao ndio watekelezaji wakuu wa mradi huo amesema kuwa Taasisi yake imejiandaa kitaalam kusimamia, kuratibu na kuhakikisha mradi huo unafanikiwa katika viwango vilivyokusudiwa.

"FETA ndio itasambaza pembejeo muhimu ikiwa ni pamoja na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki lakini pia itasimamia uwekaji wa miundombinu kama vizimba pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mradi" Amesema Dkt Mzighani. 

Fedha zilizokabidhiwa leo ni sehemu ya shilingi Bilioni 200 zilizoahidiwa kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo utekelezwaji wake utaongeza ajira zaidi za watanzania 4600 walioajiriwa kwenye viwanda 64 vya kuchakata mazao ya uvuvi nchini huku pia ikitarajiwa kuongeza uzalishaji wa samaki uliofikia takribani tani 599,199 kwa sasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani,  Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya kilimo nchini (TADB) na viongozi wengine wakiwa kwenye picha ya pamoja na vijana waliohitimu programu ya Jenga kesho iliyo bora upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) muda mfupi baada ya kuwakabidhi mfano wa hundi ya shilingi Bil. 7 kwenye hafla iliyofanyika Machi 07,2026.

Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya kilimo nchini (TADB) Bw. Mkani Waziri (kulia) akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka mfano wa hundi ya shilingi Bil.7 ambazo ni sehemu ya uwezeshwaji wa mitaji kwa vijana waliohitimu programu ya Jenga kesho iliyo bora upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) kwenye hafla iliyofanyika leo Machi 07,2026 jijini Mwanza. Wengine wanaoshuhudia kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Ghati Chomete.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani (nyuma) wakiwakabidhi  vijana waliohitimu programu ya Jenga kesho iliyo bora upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) mfano wa hundi ya shilingi Bil.7 zilizotolewa kwenye hafla iliyofanyika leo Machi 07,2026 jijini Mwanza.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO