SERIKALI KUANZISHA PROGRAMU YA MAFUNZO YA TEKNOLOJIA YA UZALISHAJI KUKU NCHINI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imeanza mchakato wa kuanzisha programu ya mafunzo ya teknolojia ya kuku ili kukidhi mahitaji ya wadau wa sekta hiyo, mchakato ambao umeanza na maandalizi ya mtaala pekee ambapo warsha ya wadau imefanyika ili kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa kuku ngazi ya Astashahada na Stashahada yenye lengo la kuanzisha programu hiyo ili kupata wataalamu mahiri watakaochangia kuleta mabadiliko makubwa katika Tasnia.

Akizungumza leo Machi 23, 2026 Jijini Dar es Salaam katika Warsha hiyo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, amesema Mafunzo ya ufugaji kuku yamekuwa yakitolewa kwa sehemu ndogo sana ndio maana sasa Serikali imeona ni vyema kuanzisha Mtaala mahususi wa kuzalisha wataalam wabobevu kwenye tasnia hiyo kutokana na uhitaji wa wadau wa sekta binafsi na ukuaji wa sekta yenyewe nchini.

"Wizara kupitia Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi imeendelea kuboresha Mafunzo ya Mifugo kupitia uhuishaji wa Mitaala ambayo ni nyenzo kuu katika kuzalisha wataalamu wa mifugo wanaohitajika nchini, na Mtaala huo utatumika kama mwongozo wa kufundishia na kuwandaa wataalamu wenye ujuzi na umahiri katika kutoa huduma kwa jamii na utawawezesha wanafunzi kupata ujuzi, ujasiri na uzoefu unaohitajika kwenye soko la ajira." amesema Mhe. Kamani.

Aidha, Mhe. Kamani amesema kazi kubwa imefanyika ya kutembelea sehemu kubwa ya wadau wa sekta ndogo ya kuku, kukusanya mahitaji na maoni yao na kuandaa maudhui ya mtaala tarajiwa, na ni dhahiri kuwa Serikali ilihitaji ushiriki mkubwa wa wadau hasa kutoka sekta binafsi ili kuhakikisha mtaala tarajiwa unajibu matakwa yote. 

Vilevile, Mhe. Kamani amebainisha kuwa mafunzo kwa kutumia Mtaala mpya yanatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa masomo, na amesema kuwa ana matumaini mafunzo yatakayotolewa kwa kutumia mtaala huo ambao unafanyiwa maboresho yanaweza kuongeza mchango mkubwa wa sekta hiyo na kwa wafugaji, pamoja na pato la Taifa, ikiwemo fursa za ajira hasa kwa vijana na wanawake nchini.

Mhe. Kamani ameweka wazi kuwa licha ya tasnia ya kuku kukumbwa na changamoto mbalimbali, Wizara imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na hizo changamoto, ikiwemo kuanzishwa dawati mahususi la sekta ndogo ya kuku katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha mnyororo mzima wa thamani wa kuku unapata msukumo wa kipekee, Kuboresha kituo cha kuzalisha chanjo kilichopo Kibaha-Mkoani Pwani ili kuzalisha chanjo za magonjwa makubwa ya kuku kama vile mdondo kwa ajili ya kuku wa asili na kisasa kwa wafugaji wote wadogo na wakubwa na kushirikiana na wadau wa sekta ya kuku kuhakiki ubora wa vyakula vya kuku na wanyama wengine wafugwao kupitia kituo maalum cha uhakiki wa vyakula vya mifugo kilichopo Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) - Temeke ili kukabiliana na tatizo la utumiaji wa vyakula visivyo na ubora.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele amesema ufanisi na utekelezaji wa mtaala huo utahitaji miundombinu  na vifaa vya kufundishia ambavyo ni adimu, na hili litawezekana kwa wadau wa tasnia kushirikiana na Wizara pamoja na LITA katika kufanikisha hilo.

Pia, Dkt. Madele amesema mtaala huo umekuja muda muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo imedhamilia kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya Mifugo ikiwemo Tasnia ya Kuku.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi (DRTE) Bi. Emelda Adam, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya Mifugo na Uvuvi Nchini, ameishukuru LITA kwa juhudi walizofanya kwa kuhakikisha inapata wadau wahususi wa kuweza kusaidia katika kupitia na kufanya maboresho ya Mtaala ambao utaleta tija kwa wafugaji kuku.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Lazaro Mwambene amesema LITA imeanza kupitia Mtaala wa Teknolojia ya uzalishaji kuku, mtaala ambao umewashirikisha wadau mbalimbali nchini ili kuweza kuboresha Mtaala huo na kuja na Mtaala wenye tija zaidi, baada ya kupitiwa na wadau na kuridhiwa nao.

Dkt. Mwambene amesema Mtaala huo mpya hautogusa kwenye kuku tu peke yake bali utazingatia teknolojia mpya za uzalishaji wa kuku wenye tija.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Kamani, akihutubia wadau wa tasnia ya kuku, katika Warsha ya Wadau wa Tasnia hiyo ya kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele, akizungumza na wadau wa tasnia ya kuku, katika Warsha ya Wadau wa Tasnia hiyo ya kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Mafunzo ya Mifugo na Uvuvi Nchini, Bi. Emelda Adam, akielezea jitihada za Wizara katika kukuza Tasnia ya Kuku kwa wadau wa tasnia hiyo, katika Warsha ya Wadau wa Tasnia ya Kuku kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Lazaro Mwambene, akielezea Mkakati wa LITA katika kuunda Mitaala mipya yenye tija kwa wafugaji, katika Warsha ya Wadau wa Tasnia ya Kuku kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam.

Mfugaji wa Kuku, Dkt. Catherine Gwandu (aliyesimama kulia), akimuelezea Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Kamani (katikati waliokaa mbele), changamoto za bei ya Mayai katika soko, katika Warsha ya Wadau wa Tasnia ya Kuku kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam.

Picha ni baadhi ya wadau wa Tasnia ya Kuku wakiwa katika Warsha ya Wadau wa Tasnia ya Kuku kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Kamani (aliyekaa mstari wa mbele katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa tasnia ya kuku, katika Warsha ya Wadau wa Tasnia hiyo ya kupitia na kuboresha Rasimu ya Mtaala wa Teknolojia ya Uzalishaji wa Kuku, Ngazi ya Astashahada na Stashahada, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Machi 23, 2026 Dar es Salaam.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO