PROF. SHEIKH AWATAKA IUCN KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA WIZARA KATIKA UTEKELEZAJI WA MRADI
Na. Stanley Brayton
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh amelitaka Shirika la Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) kuzingatia vipaumbele vya Wizara katika utekelezaji wa Mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu ili kuleta tija katika Sekta ya Uvuvi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakati wa Kikao cha kupitia Mradi wa Pamoja Tuheshimu Bahari Yetu unaoratibiwa na ICUN na kutekelezwa na Wizara za Kisekta na Taasisi zisizo za kiserikali, leo Machi 2, 2026 Mkoani Morogoro, Prof. Sheikh amewataka IUCN kuzingatia vipaumbele vya Wizara katika utekelezaji wa Mradi huo.
"ni vyema ICUN kufuata Miongozo na Taratibu za Wizara katika kutekeleza Mradi kwa kuchangia katika Mkakati wa Mageuzi wa Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji kwa mwaka 2026/2050, na programu zenu zilenge kwenye kufanya Mageuzi katika Sekta ya Uvuvi.” amesema Prof. Sheikh
Vilevile, Prof. Sheikh amesema kwa sasa Wizara inataka kufanya Mageuzi katika Sekta ya Uvuvi na ndio maana imeandaa Mpango Mkakati wa Mageuzi wa Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbemaji kwa mwaka 2026/2050, ambao utaleta mabadiliko katika Sekta ya Uvuvi kwani inaendana na Dira ya Taifa ya mwaka 2050, na ameitaka ICUN kutoa Mafunzo zaidi katika Sayansi ya Baharini na kuendelea kuwajengea uelewa wananchi ili waweze kufuga samaki kwa tija.
Pia, Prof. Sheikh amesema kwa sasa uwezo wa kuzalisha vifaranga ni mdogo kuanzia upande wa Samaki maji baridi na maji chumvi, hivyo ni vyema IUCN wakashirikiana na serikali kwa kuwa na programu ya Ukuzaji Viumbemaji wa bahari ambayo itaenda kusaidia katika Uzalishaji wa vifaranga kwa wingi.
Prof. Sheikh amesema Wizara inaunga mkono juhudi za ICUN na inahaidi kutoa ushirikiano wa kotosha kwao, kwani inasaidia katika kuhifadhi rasilimali za uvuvi katika ukanda wa pwani, kusaidia Taasisi za Wizara (MPRU na TAFIRI) kupitia programu za kuhifadhi maeneo tengefu, kutoa vifaa vya utafiti, kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosababisha na utupaji holela wa taka za plasti, uhifadhi mikoko, pamoja na kutoa ufadhili katika ngazi za Uzamili na Uzamivu.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Pamoja Tuheshimu Bahari Yetu kutoka IUCN, Dkt. Mathias Igulu, akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mradi huo kwa Mwaka 2026 pamoja na mambo mengine, amefafanua kwamba mradi umetoa ufadhili kwa wanafunzi 28 wa ngazi za Uzamili na Uzamivu ambao wataenda kuwa chachu katika Sekta ya Uvuvi.




Maoni
Chapisha Maoni