MKANDARASI WA GHALA LA UBARIDI TAFICO ATAKIWA KUKAMILISHA KAZI KWA WAKATI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena, ameiagiza kampuni ya Kabirirti Engineering Limited inayotekeleza mradi wa ukarabati wa ghala la ubaridi (Cold Storage) la Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Prof. Sheikh ametoa agizo hilo leo Machi 9, 2026 wakati alipotembelea Makao Makuu ya TAFICO yaliyopo Ras Mkwavi-Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua miundombinu ya uhifadhi wa samaki na mazao ya uvuvi.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kwa wakati ni muhimu katika kuimarisha shughuli za uvuvi na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao ya baharini, jambo litakalosaidia kuongeza thamani ya bidhaa za uvuvi pamoja na kuchochea uchumi wa sekta hiyo.
Kwa upande wake, mkandarasi wa mradi huo kutoka Kabirirti Engineering Limited ameeleza kuwa kazi ya ukarabati inaendelea vizuri na kwamba watahakikisha wanazingatia maelekezo yaliyotolewa ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa.
Mradi wa ukarabati wa ghala hilo la ubaridi ulianza mapema mwezi Februari 2026 na unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 90 tangu ulipoanza. Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza uwezo wa TAFICO kuhifadhi samaki na mazao mengine ya uvuvi katika mazingira salama na yenye viwango vinavyokubalika kimataifa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya uvuvi ili kuhakikisha inaleta tija inayotarajiwa kwa taifa.
Pia katika Ziara hiyo Prof. Sheikh alishiriki kikao na mdau wa maendeleo Bw. Kim Bong-Jo kutoka kampuni ya Galleon Korea Co. LTD ya nchini Korea Kusini, inayolenga kufanya uwekezaji wa pamoja na TAFICO.

Maoni
Chapisha Maoni