MHE. KAMANI AITAKA FETA KUONGEZA UZALISHAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI
Na. Stanley Brayton, WMUV
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki kutoka kiwango cha sasa na kufikia kati ya milioni 5 hadi 10 kwa mwezi, ili kuchochea ukuaji wa Sekta ya uvuvi na kuongeza tija kwa wananchi.
Akizungumza leo Machi 5, 2026 jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Tatu ya Ushauri ya FETA, Mhe. Kamani amesema kuwa ongezeko la uzalishaji wa vifaranga litasaidia kuimarisha shughuli za ukuzaji viumbemaji na kuongeza mchango wa Sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa.
"Bodi mpya inapaswa kusimamia kwa karibu Mpango Mkakati wa Wakala, na kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za samaki, pamoja na kushirikiana na Taasisi nyingine zikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), katika kuanzisha Mpango wa Kitaifa wa kuboresha mbegu za mazao ya viumbe
maji" amesema Mhe. Kamani.
Aidha, Mhe. Kamani amewataka wajumbe wa Bodi hiyo kuimarisha mafunzo ya vitendo kwa vijana kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT - Uvuvi) ili kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa Buluu.
Katika hafla hiyo, Mhe. Kamani amezindua rasmi Bodi ya Tatu ya Ushauri ya FETA na kusisitiza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuiwezesha sekta ya uvuvi kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena amesema ili kuendeleza tasnia hiyo ya Uvuvi kwa njia endelevu, Wizara inahitaji wataalamu wenye ujuzi stahiki, ambao wanapatikana kupitia FETA.
Vilevile Bi. Meena amempongeza mwenyekiti na wajumbe wote wa Bodi Kwa kuteuliwa, na kuwapongeza Kwa dhumuni la kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Tatu ya Ushauri ya FETA, Dkt. Blandina Lugendo amesema malengo ya FETA yatatekelezwa kikamilifu na weledi, na pia ameiomba Wizara iweze kuwajengea miundombinu mipya ya kuweza kuendesha Taasisi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Isa Mzighani amesema jukumu kuu la FETA ni kutoa elimu juu Ukuzaji Viumbe maji, pia wamepewa jukumu la kuboresha miundombinu ya Kampasi za Uvuvi ili kutoa wataalamu watakaosimamia bandari za uvuvi na kuanzisha kozi ya kimataifa ya uangalizi wa bandari.







Maoni
Chapisha Maoni