MAFUNZO REJEA YA MAAFISA UGANI YAZINDULIWA NCHINI

Na. Fausta Njelekela

◾Wizara kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa kununua pikipiki 200.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi yaanza kutoa Mafunzo rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi ambapo mafunzo hayo yenye lengo la kuwafundisha maafisa Ugani masuala mbalimbali ikiwemo kuzingatia ufugaji na uvuvi endelevu, usimamizi endelevu wa rasilimali za mifugo na uvuvi pamoja na sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamia sekta za mifugo na uvuvi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hafla hiyo iliyofanyika Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma Machi 3, 2026, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele amesema mafunzo hayo ni moja ya hatua na mikakati iliyowekwa na wizara ya kuhakikisha inaimarisha huduma za ugani kwa kutoa mafunzo rejea kwa maafisa ugani ili kujenga uelewa wa pamoja katika masuala mbalimbali ya kitaalamu yanayolenga kuongeza tija katika uzalishaji ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa yanayolenga kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umasikini.

"Ni matumaini yangu kuwa katika siku hizi mbili mtapata nafasi ya kujadiliana kwa kina na kwa uwazi kuhusu namna ya kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu ya sekta hizi na tujikite katika kuboresha utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati, kusambaza teknolojia bora na bunifu zinazoongeza tija, kuimarisha elimu kwa wafugaji na wavuvi, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu unaozingatia viwango na miongozo iliyopo.  .” amesema Dkt. Madele

Aidha, Dkt. Madele, amesema mafunzo haya yawe jukwaa la kutathmini changamoto, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji huduma za ugani ambazo zina mchango mkubwa katika kusaidia kufanya mageuzi ya sekta za mifugo na uvuvi.

Vilevile, Dkt. Madele amebainisha kuwa mabadiliko ya kisayansi na kitekinolojia katika uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi yameleta msukumo kwa wizara kuandaa mafunzo kama hayo ili kuwawezesha maafisa ugani kutoa huduma hii kwa ufanisi.

Pia, Dkt. Madele amesema Maafisa Ugani kutoka katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wana mchango mkubwa katika utoaji wa huduma na ushauri kwa wafugaji na wavuvi katika nchi yetu ili kukuza sekta hizi. 

Hivyo, Dkt. Madele amewataka Maafisa Ugani kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kuwa wao ndio kiungo kikuu katika kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu, na Miongozo ya sekta.

Dkt. Madele amesema katika kuendelea kutatua changamoto ya utoaji wa huduma za Ugani, kuanzia mwaka 2023-2025 wizara imenunua jumla ya pikipiki 2,258 na kuzisambaza kwa Maafisa Ugani nchini na imenunua na kusambaza vishikwambi 4,500; vifaa vya chanjo ikiwemo cool box (3,270), automatic syringe (3,270), gumboots (2,180); na Overoli (2,18), na bado katika mwaka 2025/2026 wizara itaendelea  kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa kununua pikipiki 200 ambazo zitasambazwa kwa maafisa ugani nchini; na kutoa mafunzo rejea.  

Dkt. Madele, ametoa rai kwa Maafisa Ugani kujenga ushirikiano wa karibu, wa heshima na wa kudumu kati yao na wafugaji pamoja na wavuvi ambao ndio walengwa wa huduma. Mahusiano hayo yajengwe katika misingi ya uaminifu, mawasiliano ya wazi na utatuzi wa changamoto, ili kuharakisha maendeleo ya sekta na kufikia malengo ya wizara kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Ndg. Tito Mganwa ameishukuru wizara na kusema kuwa mafunzo hayo ni muhimu na yataleta chachu katika kukuza sekta zote mbili wilayani hapo.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina amesema ni vyema Maafisa Ugani kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuleta tija katika sekta zote mbili za mifugo na uvuvi kwa kuwahudumia wananchi.

Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa na wizara za kuwajengea uwezo wataalam wa mifugo na uvuvi katika kutekeleza majukumu ya utoaji wa huduma za ugani nchini. Mafunzo kama haya yamekuwa yakitolewa ambapo mpaka sasa jumla ya maafisa ugani 1,908 wamepatiwa mafunzo katika kipindi cha 2022 – 2025 kati ya maafisa 4,959 waliopo.

Mafunzo haya yanategemewa kuendelea katika mikoa mingine kuanzia tarehe 3 hadi 14 Machi, 2026 katika kanda nne (4) za Kati (Chamwino – Dodoma); Nyanda za Juu Kusini (Makambako – Njombe); Mashariki (Mkuranga – Pwani); na Ziwa (Chato – Geita).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele, akihutubia Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja  na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Ndg. Titto Mganwa, akizungumza na Maafisa Ugani wa Mifugo nw Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (DARHAM), Dkt. Charles Mhina, akizungumza na Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma.
Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi (DRTE), Bw. Samwel Mdachi, akizungumza na Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma.
Picha ni Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele (hayupo pichani), wakati wa Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma.
Picha ni Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi wakiendelea na Mafunzo, baada ya Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Madele (aliyekaa mstari wa mbele katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Machi 3, 2026 Dodoma, wa kwanza kushoto ni Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bw. Elisante Saktay.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO