MAAFISA UGANI WAHIMIZWA KUBADILISHANA UZOEFU ILI KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI

Wataalamu wa ugani wa sekta za mifugo na uvuvi kutoka Kanda ya Ziwa wameanza mafunzo rejea katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita leo Machi 9, 2026, yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa wafugaji na wavuvi.

Akifungua mafunzo hayo, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe Lois Bura amewahimiza maafisa ugani kubadilishana uzoefu na kutumia ujuzi wao wa kitaalamu ili kuboresha huduma wanazozitoa kwa wananchi, hususan wafugaji na wavuvi  wanaotegemea ushauri wao katika shughuli za uzalishaji.

"Maafisa ugani ni kiungo muhimu katika kufikisha sera, sheria na teknolojia bora za ufugaji na uvuvi ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuendelea kuimarisha usalama wa chakula na kipato kwa wananchi." amesema Mhe. Bura

Aidha, Mhe. Bura amesema kuwa huduma za ugani zina mchango mkubwa katika kuleta mageuzi  kwa kusaidia kupeleka mbinu na teknolojia mpya kwa wafugaji pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ndg. Joshua Elisha ambaye ni Afisa Tawala Mkuu amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa juhudi za wizara za kuwajengea uwezo wataalamu wa mifugo na uvuvi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika utoaji wa huduma za lugani nchini.

Vilevile Ndg. Elisha ameongeza kuwa mafunzo hayo yanawakutanisha maafisa ugani kutoka ngazi mbalimbali ikiwemo mikoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa ambapo washiriki wanapata fursa ya kujifunza mada mbalimbali zinazohusu uzalishaji wa mifugo, udhibiti wa magonjwa pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwasaidia wataalamu kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wafugaji na wavuvi nchini.

Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Lois Bura (aliyesimama mstari wa mbele katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, baada ya Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Kanda ya Ziwa na Magharibi  kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa IFM Machi 9, 2026 Chato

Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Lois Bura, akihutubia Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi  yaliyofanyika katika Ukumbi IFM, Machi 9, 2026 Chato.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Ndg. Joshua Elisha Afisa Tawala Mkuu, akitoa neno la utangulizi Kwa  Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa Sekta hizo, katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi yaliyofanyika katika Ukumbi IFM, Machi 9, 2026 Chato.

Dkt. Vayan Levanoi Laizer (wa kwanza kulia) kutoka wizara ya mifugo na uvuvi akiwaelezea maafisa ugani mada inayohusu huduma za wanyama na magonjwa ya wanyama , katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi  yaliyofanyika katika Ukumbi wa IFM, Machi 9, 2026 Chato

Picha ni Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi, wakimsikiliza Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Lois Bura (hayupo pichani), katika Hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, yaliyofanyika katika Ukumbi wa IFM, Machi 9, 2026 Chato.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

DKT. MHEDE AONGOZA ZOEZI LA UCHANJAJI WA MIFUGO MKOANI IRINGA, WAFUGAJI WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI

SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO