MAAFISA UGANI MIFUGO NA UVUVI TATUENI CHANGAMOTO ZA WAFUGAJI NA WAVUVI KITAALUMA - BI. MAYEMBA
Na. Stanley Brayton
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, ambaye ni Mkuu wa Idara ya usafi na uthibiti wa taka ngumu, Bi. Appia Mayemba amewataka Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi kutatua changamoto mbalimbali kitaaluma ambazo zinawakumba wafugaji na wavuvi ili kuongeza tija katika Sekta hizo za Uzalishaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Makambako wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mafunzo Rejea kwa Nyanda za Juu Kusini kwa Maafisa Ugani wa Mifugo na Uvuvi Nchini, leo Machi 9, 2026, Wilayani Makambako Mkoani Njombe, Bi. Mayemba amesema Maafisa Ugani wanapopata Mafunzo hayo mbalimbali ya Ugani na baada ya kutoka kwenye Mafunzo ni vyema kwenda kuwahudumia wafugaji na wavuvi ili kuweza kuzitatua changamoto zao kwa umakini na utulivu.
"Kama kuna jambo lolote ni vyema kushirikisha uongozi wa juu ikiwemo Wakurugenzi wa Idara mbalimbali ili kutatua changamoto za wafugaji na wavuvi kwa lengo la kupunguza masononeko kwa Serikali pamoja na uharibifu wa Mali zao.” amesema Bi. Mayemba
Aidha, Bi. Mayemba amewataka Maafisa Ugani kuwa na heshima na utulivu kwa wananchi na kufanya kazi kwa ufanisi na uweledi ili wananchi wapate mafanikio katika Mifugo yao na Uvuvi na kuipenda Serikali yao.
Vilevile, Bi. Mayemba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake nzuri katika kukuza Sekta za Mifugo na Uvuvi, na kuwataka Maafisa Ugani kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais kwa kuboresha shughuli zao kwa kuwahudumia wananchi vizuri ili kuleta tija kwenye Sekta hizo.
Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Naibu Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dkt. Obed Nyasebwa amebainisha kuwa lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa Ugani ili kuongeza ufanisi katika Utendaji kazi zao za kila siku, na Wizara inategemea baada ya Mafunzo haya ufanisi wao utaongezeka.
Pia, Dkt. Nyasebwa amesema Mafunzo haya kwa awamu hii yanalenga kuwapatia Ujuzi Maafisa Ugani 500 nchini ambao watatoka Halmashauri mbalimbali, zikiwemo Halmashauri zilizopo Mikoa ya Nyanda za juu kusini.
Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba Bi. Regina Baha amesema mafunzo hayo yaliyotolewa yamewapa faida sana hasa katika kujua namna ya kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo, pamoja na faida za kujisajili katika Baraza la Veterinari Tanzania (VCT).






Maoni
Chapisha Maoni