DKT. BASHIRU AZINDUA VITUO VYA KUKUSANYIA MAZIWA VYENYE THAMANI YA BIL. 1.157
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Bashiru Ally Kakurwa, amezindua vituo vya ukusanyaji wa maziwa vilivyojengwa kupitia mradi wa TI3P, uliogharamiwa na Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Heifer International.
Uzinduzi huo umefanyika Machi 2, 2026 mkoani Kagera, ukihusisha kituo cha kukusanyia maziwa cha Maruku kilichopo Manispaa ya Bukoba, Kituo cha Nshamba kilichopo Wilaya ya Muleba pamoja na kukabidhi mitamba 110 ya ngo’mbe wa maziwa kwa wanawake na vijana wilayani Karagwe.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Bashiru amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, anasisitiza kuwa wazalishaji wadogo, wakiwemo wafugaji na wavuvi, wanawezeshwa ili kuongeza uzalishaji wenye tija.
“Mhe. Rais alivyoniteua aliniambia, sekta hizi unazokwenda kuziongoza zinawahusu wanaovuja jasho ambao ni wazalishaji wadogo; lazima utafute mbinu za kuwaunganisha ili waongeze uzalishaji. Naipongeza benki ya TADB kwa kuja na mradi huu. Wafugaji wetu walikuwa wanamwaga maziwa kutokana na ukosefu wa miundombinu mizuri na masoko,” amesema Dkt. Bashiru.
Aidha, amesisitiza kuwa uendeshaji wa mradi huo ujikite katika kuleta mabadiliko makubwa kwa wazalishaji wadogo wa tasnia ya maziwa nchini na kuhamasisha ufugaji wa kisasa. Amewahakikishia wafugaji kuwa Wizara yake kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania itaendelea kuwaunga mkono wadau wote wa tasnia ya maziwa.
“Mpango wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa lazima uendane na upatikanaji wa malisho, maji na ardhi kwa ajili ya mifugo. Vilevile, ni muhimu kuzingatia afya ya mifugo na miundombinu bora ili kukuza tasnia ya maziwa nchini,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dkt. Abel Nyamahanga, ameishukuru Wizara kwa kushirikiana na TADB katika utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa utaongeza mapato kupitia ongezeko la uzalishaji na kukuza viwanda vya maziwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyambundege, amesema benki hiyo imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 1.157 kwa ajili ya ujenzi wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa pamoja na miundombinu yake.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Heifer International, Bw. Mark Tsosho, amesema shirika hilo limewawezesha wafugaji milioni 1.38 kufuga kisasa, na kupitia mradi wa TI3P takribani wafugaji 900,000, wakiwemo wanachama wa vyama vya ushirika 74, watanufaika kote nchini.
Naye, Msajili wa Bodi ya Nyama Prof. George Msalya amesema kaya milioni mbili nchini zinajishughulisha na uzalishaji wa maziwa, hivyo kupitia vituo vya ukusanyaji wa maziwa wafugaji watanufaika kuwa na soko la uhakikika, bei yenye tija na uhifadhi salama wa maziwa jambo litakaloongeza kipato chao.




Maoni
Chapisha Maoni